Balinya aendelea kucheka na nyavu Yanga

Friday July 19 2019

 

By Mwandishi wetu

YANGA imeendelea kuvuna ushindi katika mchezo wa pili wa majaribio wakishinda mabao 2-0 dhidi ya Moro Kids.
Mabao ya mshambuliaji Juma Balinya na beki Paul Godfrey 'Boxer'  yaliyofungwa kipindi cha kwanza yalitosha kuipa ushindi huo Yanga iliyopiga kambi yake mjini Morogoro.
Katika mchezo huo Balinya aliipatia Yanga bao la kwanza  dakika ya 15 kwa njia ya penalti akifunga kiufundi na kuitanguliza timu yake.
Penalti hiyo ilitokana na winga wa kushoto Patrick Sibomana kuangushwa ndani ya eneo la hatari wakati akitaka kufunga.
Bao hilo la Balinya ni la pili baada ya kufunga bao moja katika mchezo wa kwanza dhidi ya Tanzanite Kombaini wakati Yanga ikishinda bao 10-1.
Dakika 10 baadaye Boxer aliipatia Yanga bao la pili akiwatoka mabeki na kuachia shuti kali lililojaa moja kwa moja wavuni akipokea pasi safi ya winga mkongwe Mrisho Ngassa.
Katika mchezo huo, kocha Noel Mwandila alibadilisha kikosi ambapo dakika 45 za mwanzo kilicheza kikosi kimoja na kipindi cha pili aliingiza kikosi kingine.

Advertisement