Balinya,Sibomana washika ushindi wa Yanga kwa Zesco

Thursday September 12 2019

 

By Charles Abel

ACHANA na mkakati wa viongozi na mashabiki wa Yanga kuingia uwanjani wakiwa na vipensi kama ishara ya kumuunga mkono kocha wao, Mwinyi Zahera, lakini Yanga inajipanga vilivyo nje na ndani ya uwanja kuhakikisha inaibuka na ushindi mnono dhidi ya Zesco United kwenye mechi baina yao itakayochezwa keshokutwa Jumamosi katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Nje ya Uwanja, Yanga imeanza kampeni ya kuhamasisha mashabiki wake na Watanzania kijumla kujaa kwa wingi uwanjani hapo keshokutwa kwa kuweka kiingilio cha chini Sh3,000 ili waweze kuwapa sapoti na hamasa nyota wake, pia kuwavuruga kisaikolojia wapinzani wao.

Pia upande wa maandalizi ya kiufundi, Yanga ilijichimbia huko jijini Mwanza kuandaa mipango na mbinu za kuwamaliza Wazambia hao huku ikicheza mechi mbili za kirafiki kwa ajili ya kupima ufanisi wa kile ilichokifanyia kazi kwenye maandalizi hayo.

Mashabiki watashuhudia soka lenye ushindani wa hali ya juu kutoka kwa timu zote na bila shaka zitaufungua uwanja kwa ajili ya kusaka ushindi na sio mojawapo kupaki basi.

Hata hivyo, mechi hiyo huenda ikanogeshwa zaidi na vita tano za ndani ya uwanja baina ya wachezaji wa timu hizo mbili na bila shaka upande utakaofanikiwa kuibuka mshindi, utakuwa kwenye nafasi kubwa ya kuondoka kifua mbele kwenye mechi hiyo. Vita ya kwanza itakuwa ni baina ya beki kisiki wa Yanga na Taifa Stars, Kelvin Yondani dhidi ya mshambuliaji Jesse Were wa Zesco.

Yondani anasifika kwa uwezo wake wa kutia mfukoni washambuliaji wa timu pinzani kutokana na hesabu zake sahihi pindi anapowania nao mpira, uwezo wa kuwapora mipira na uwezo wa kumiliki mpira mguuni lakini atakutana na kipimo cha Were ambaye anajua vyema kutumia umbo lake katika kufumania nyavu kwa kutumia kichwa na miguu, uwezo wa kuwatoka mabeki na kupiga pasi za mwisho.

Advertisement

Ukiondoa vita hiyo, nyingine itakuwa ni ile ya mshambuliaji wa Yanga, Juma Balinya ambaye ni raia wa Uganda dhidi ya beki Mkenya, David Owino.

Balinya ni mjanja wa kukaa kwenye nafasi na kufumania nyavu, pia ana uwezo mkubwa wa kupiga pasi za mwisho na kuwatoka mabeki wa timu pinzani lakini atakutana na Owino ambaye ni mtulivu na asiye na papara pindi anapokabilina na mshambuliaji wa timu pinzani akitumia vyema umbo lake na akili kuokoa mipira inayoelekezwa lango mwaka iwe ya chini au ya juu.

Beki mwingine wa kati wa Yanga, Moro Lamine ambaye amejizolea umaarufu mkubwa katika siku za hivi karibuni yeye atakuwa na kibarua kigumu mbele ya mshambuliaji Umaru Kasumba.

Moro ni mchezaji anayecheza kwa nidhamu ya hali ya juu kimbinu na anajua kuipanga vyema timu pamoja na kufuta makosa ya kwenye safu ya ulinzi na yeye ndio anategemewa kwa kiasi kikubwa kumdhibiti straika anayejua kufumania nyavu, Umaru Kasumba ambaye amenaswa na Zesco kabla ya kuanza msimu huu akitokea Sofapaka ya Kenya alikopachika mabao 19 msimu uliopita.

Katikati mwa kiwanja kutakuwa na ushindani mkubwa baina ya nahodha wa Yanga, Papy Tshishimbi na kiungo Mkenya wa Zesco United, Anthony Akumu.

Uwezo wa Tshishimbi katika kuunganisha timu na kuichezesha pamoja na kuifungua safu ya kiungo ya timu pinzani unategemewa na Yanga kuwa silaha kwenye mechi hiyo ya Jumamosi lakini ana kazi kubwa mbele ya kiungo mkabaji wa Zesco, Akumu ambaye ni fundi wa kung’amua na kutibua mipango ya timu pinzani lakini pia kupora mipira na kuchezesha timu.

Vita ya mwisho ni ile itakayokuwa baina ya viungo Mohamed Issa ‘Banka’ wa Yanga na Thaban Kamusoko wa Zesco.

Kamusoko ni mchezaji anayeweza kuchezesha vyema timu na kuiunganisha akibebwa na uwezo wake wa kupiga pasi zinazofikia walengwa kwa usahihi, utulivu, kuzisoma timu pinzani, pia kupiga pasi za mabao ingawa pia anaweza kufunga pindi apatapo nafasi.

Nyota huyo kutoka Zimbabwe, aliwahi kuichezea Yanga msimu uliopita na bila shaka anaifahamu vyema jambo ambalo huenda likampa wakati mgumu Banka ambaye ni mchezaji anayemudu vyema kucheza kama kiungo wa chini.

Banka anajua kujipanga kwenye nafasi sahihi uwanjani na kuziba njia za wapinzani kupitisha mpira kwenda langoni mwake lakini pia anaweza kuchezesha timu. Lakini mbali na vita hivyo baina ya wachezaji ndani ya uwanja, Yanga ina nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi ikiwa itafanyia kazi ya mambo kabla ya mchezo huo.

Kwanza ni kuwa na mshambuliaji mmoja wa kati wa kusimama karibu na lango la Zesco ili awalazimishe mabeki wa timu hiyo kutoanzisha mashambulizi kutokea nyuma, kuwanyima uhuru pamoja na kuwa karibu na mipira itakayosambaa kwenye eneo la hatari pindi watakapokuwa wanashambulia.

Pili ni kuhakikisha inakamata safu ya kiungo ya Zambia ambayo ndio imekuwa uti wa mgongo wa kupika mashambulizi na mabao ya timu hiyo. Kiuhalisia Zesco mara kwa mara imekuwa ikitumia mfumo wa 4-4-2, lakini huwa haina mawinga asilia bali hwaanzisha viungo wawili washambuliaji kucheza upande wa wingi ya kushoto na kulia jambo linalofanya wawe imara zaidi katikati.

Kocha na mchambuzi wa soka, Joseph Kanakamfumu alisema Yanga inapaswa kufanya kazi kubwa zaidi kwenye mechi hiyo dhidi ya Zesco kwani wachezaji wake hawana muunganiko mzuri kuliko wapinzani wao.

“Zesco wachezaji wake wengi wamekaa pamoja kwa muda mrefu. Timu yao ni ileile ambayo imefanya vizuri miaka michache iliyopita na kama kuondoka au kuingia kikosini basi ni wachezaji wachache tu. Munnganiko wao wa kiuchezaji uko vizuri na wamezoeana.

Eneo litakalowapa shida zaidi nahisi ni katikati ambayo hadi sasa hajapata safu ya kudumu. Pia Papy Tshishimbi amekuwa hana nidhamu ya kimbinu ya kucheza kwenye nafasi yake jambo ambalo linamfanya Mohamde Banka awe anashuka kumzibia nafasi yake jambo linalopelekea washambuliaji wakose huduma sahihi,” alisema Kanakamfumu.

Mshambuliaji wa Coastal Union, Ayoub Lyanga ambaye aliwahi kuchezea Zanaco FC, alisema Yanga inapaswa kuwa makini na Zesco kwani haimtegemei mchezaji mmojammoja. “Zesco wana timu nzuri na ina wachezaji wengi ambao wana viwango vya juu hivyo Yanga inapaswa kujiandaa vilivyo kuwakabili. Hawapaswi kufanya makosa ya mara kwa mara na wasiwape nafasi ya kumiliki mpira,” alisema Lyanga.

Advertisement