Bale anakopeshwa kwa Pauni 10 mil

Thursday May 16 2019

 

MADRID, HISPANIA.GARETH Bale hatakiwi huko Real Madrid na klabu yake ya zamani ya Tottenham Hotspur imeambiwa ikamchukue kwa mkopo wa Pauni 10 milioni.

Kinachoelezwa ni kwamba Real Madrid inataka sana kumwondoa mchezaji huyo kwenye kikosi chake hasa baada ya Zinedine Zidane kuonekana wazi kuwa hamtaki. Wababe hao wa Bernabeu wanataka kujinasua kwenye shida ya mshahara mkubwa wanaomlipa mchezaji huyo huku mwenyewe akigoma kung’atuka kuacha pesa ndefu kiasi hicho, Pauni 600,000 kwa wiki.

Sasa Madrid ipo tayari kumtoa kwa mkopo kwa timu itakayokuwa tayari kulipa mshahara wa Pauni 250,000 kwa wiki ikitoa Pauni 10 milioni, basi itamchukua mchezaji huyo.

Bale amekuwa adui namba moja wa mashabiki wa Real Madrid wakimzomea mchezaji huyo kiasi cha kumfanya Kocha Zidane kumwondoa kikosini kwenye mechi za karibuni.

Spurs imeambiwa ikamchukue mchezaji wake huyo iliyemuuza kwa ada iliyovunja rekodi ya dunia mwaka 2013 ya Pauni 86 milioni. Lyon pia inamtaka Bale kwa mkopo, lakini shida inakuja kwenye kumudu mshahara wa Pauni 250,000 kila wiki. Manchester United ilitajwa kumtaka mchezaji huyo, lakini shida inakuja kama Real Madrid itakuwa tayari kumpeleka kwa mkopo huko Old Trafford.

Wakala wa Bale, Jonathan Barnett alisema mchezaji wake ataendelea kubaki Real Madrid na kwa muda wa mkataba wake uliobaki utamshuhudia akipokea Pauni 100 milioni hata kama hatakuwa akicheza.

Advertisement