Balaa la long na mastaa England

Muktasari:

  • England na hivyo kuvunja rekodi za watu kibao zilizodumu kwa miaka mingi. Hii hapa ndio orodha ya mabao yaliyofungwa haraka zaidi kwenye historia ya Ligi Kuu England.

LONDON, ENGLAND.LIGI Kuu England inatambulika kama moja ya ligi isiyotabirika kuliko nyingine zote tano za Ulaya na msimu huu wa 2018/19 imekuwa ikiwafanya mashabiki kukumbana na mambo mengi yenye kuwashangaza na kuwaacha vichwa wazi.

Liverpool na Manchester City zenyewe ndio zimekuwa zikichuana jino kwa jino kwenye kufukuzia ubingwa wa msimu huu huku kukiwa na timu nne zinazopigania nafasi mbili ya tatu na nne ili kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Wakati ligi hiyo ikiwa na sifa ya kucheza kwa kasi na mabao ya kutosha kuna timu zimekuwa zikijaribu kufanya mambo makubwa katika kila msimu, lakini kwa sababu ligi hiyo imekuwa na mambo mengi ya kushtukiza yanayotokea bila kupangwa ikiwamo mabao ya haraka zaidi.

Usiku wa juzi Jumanne, Shane Long aliingia kwenye rekodi tamu kabisa ya kuwa mchezaji aliyefunga bao la mapema zaidi katika historia ya Ligi Kuu England na hivyo kuvunja rekodi za watu kibao zilizodumu kwa miaka mingi. Hii hapa ndio orodha ya mabao yaliyofungwa haraka zaidi kwenye historia ya Ligi Kuu England.

5. Mark Viduka vs Charlton, sekunde 11.90

Mark Viduka alikuwa straika mwenye ufundi mkubwa sana ambapo aliucheza mpira kwa madaha makubwa kiasi cha kumfanya awe kipenzi cha watu wengi waliokuwa wakimtazama akicheza na kufurahia soka lake. Viduka kipindi hicho akitamba kwenye Ligi Kuu England akiwa na kikosi cha Leeds United alikuwa akifunga mabao matamu kwelikweli.

Katika kipindi chake cha misimu minne aliyokuwa katika kikosi cha Leeds alifunga mabao 72 katika michuano yote aliyotumikia wababe hao wa Elland Road. Lakini, moja ya mabao yake Viduka yameacha rekodi kwenye Ligi Kuu England kwa kuingia kwenye rekodi ya kufungwa mapema zaidi wakati alipofanya hivyo dhidi ya Charlton Athletic katika msimu wa 2000/01. Katika mechi hiyo, Viduka alitumia sekunde 11 tu kufunga bao la kwanza kwenye mechi hiyo ya ligi baada ya kupokea pasi ya kichwa kutoka kwa Alan Smith, ambaye aliunganisha vyema pasi ya Ian Harte.

4. Christian Eriksen vs Man United, sekunde 10.54

Tottenham Hotspur kwa miaka ya karibuni wakiwa chini ya kocha Mauricio Pochettino wamekuwa na kawaida ya kuwapa presha wapinzani wao na kuhakikisha wanafunga mabao katika mazingira ambayo ni ngumu kuamini kama bao lingepatikana.

Katika msimu wa 2017/18 staa wao Christian Eriksen aliingia kwenye rekodi za kuwa mmoja wa wachezaji waliofunga mabao ya mapema kwenye historia ya Ligi Kuu England baada ya kutumia sekunde 10.54 tangu filimbi ya kuanza mchezo ilipopulizwa na kufunga bao katika mechi dhidi ya Manchester United.

Baada filimbi ya kuanzisha mechi kupulizwa, mpira mrefu uliopigwa mbele, uligongwa kichwa na Harry Kane kumfikia Dele Alli, aliyeachia shuti kali lakini likazuiwa na beki Chris Smalling kabla ya mpira huo uliozuiwa kumfikia Eriksen na kupiga golini ukimshinda kipa David de Gea kuwafanya Spurs kufunga bao la kwanza kwenye sekunde ya 10 ya mchezo.

3. Alan Shearer vs Man City, sekunde 10.52

Katika msimu wa 2002/03 mechi ya Newcastle United na Manchester City yani ile refa anapuliza filimbi ya kuanzisha mechi, hata sekunde 11 hazifafika, supastaa mwenye mabao yake kwenye Ligi Kuu England, Alan Shearer aliwarudisha kati Man City kuja kuanza upya mchezo baada ya kuwafunga bao matata.

Kipindi hicho kipa wa Man City alikuwa Carlo Nash na hakika yeye anaweza kuwa na kumbukumbu nzuri ya kuingia kwenye orodha ya makipa waliofungwa mabao ya mapema zaidi kwenye historia ya Ligi Kuu England. Shearer alimfanya vibaya kipa Nash na kisha kuja kufunga bao akiwa yeye na nyavu tu kuipatia Newcastle United bao la kuongoza katika sekunde ya 10.52.

2. Ledley King vs Bradford City, sekunde 09.82

Katika msimu wa 2000/01, beki wa kati Ledley King aliweka rekodi ya kuwa mchezaji aliyefunga bao la mapema zaidi kwenye Ligi Kuu England kabla ya Shane Long kuja kuvunja rekodi yake usiku wa juzi Jumanne. Utashangaa kwa miaka 19, rekodi ya bao la mapema kwenye Ligi Kuu England ilikuwa ikishikiliwa na beki na si mchezaji wa safu ya ushambuliaji.

Lakini, kwa kipindi hicho, King alikuwa akicheza kwenye sehemu ya kiungo. King alifunga kwenye mechi dhidi ya Bradford City ambapo baada ya mechi tu kuanza mpira uliopigwa kwenye nusu ya timu hiyo kuna mchezaji alijaribu kuupiga kichwa ili uondoke kwenye eneo la hatari, lakini mpira huo ulitua kwenye miguu ya King, ambaye hakufanya mzaha na kukwaamisha mpira nyavuni. Kipindi hicho King alikuwa akikipiga kwenye kikosi cha Tottenham Hotspur.

1. Shane Long vs Watford, sekunde 07.69

Straika wa Southampton, Shane Long amevunja rekodi ya beki Ledley King iliyodumu kwa miaka 19 ya kufunga bao la mapema zaidi kwenye historia ya Ligi Kuu England. Long, juzi Jumanne usiku alifunga bao sekunde ya saba tu katika mechi dhidi ya Watford iliyomalizika kwa sare ya 1-1, wakati Southampton ilipokuwa kwenye uwanja wa ugenini.

Baada ya filimbi tu ya kuanzia mpira, Shane Long akilimbia mbio kwenda kwenye beki ya Watford na kutumia baada ya mpira uliokolewa na Roberto Pereyra kumfikia mfungaji ambaye hakufanya makosa na kuuweka wavuni kuandika historia ya kufunga bao la mapema zaidi katika Ligi Kuu England baada ya kutulia na kumchambua kipa Ben Foster.