Baba yake Aubameyang azua utata Arsenal

LONDON, ENGLAND. PRESHA inapanda, presha inashuka. Mashabiki wa Arsenal wamekumbwa na wasiwasi mkubwa wa kumpoteza straika wao namba moja, Pierre-Emerick Aubameyang baada ya baba wa mchezaji huyo kusema kwamba mwanaye anaondoka.

Aubameyang, akiwa na umri wa miaka 31 atamaliza mkataba wake kwenye kikosi cha Arsenal mwishoni mwa msimu ujao na hakuna makubaliano yoyote ya kuhusu dili jipya yaliyofikiwa na wakali hao wa Emirates.

Wasiwasi mkubwa umekuwa kubwa juu ya hatima ya mshambuliaji huyo kuhusu kubaki Arsenal, Barcelona wakidaiwa kuendelea kufukuzia huduma yake wakitaka akakipige Nou Camp msimu ujao.

Kwenye mchezo wa mwisho wa kumaliza msimu, Aubameyang alifunga mara mbili katika ushindi wa 3-2 iliyopata Arsenal dhidi ya Watford na hivyo kushindwa kunyakua Kiatu cha Dhahabu kwenye Ligi Kuu baada ya msimu uliopita kubeba sambamba na Mohamed Salah na Sadio Mane wa Liverpool, walipofunga mabao 22 kila mmoja. Msimu huu pia, Aubameyang alifunga mabao 22, moja nyuma ya mshindi, Jamie Vardy.

Baba yake, Aubameyang, Pierre-Francois, alitumia ukurasa wake wa Instagram kumpongeza mwanaye na baada ya hapo, aliweka maneno yaliyoibua hofu kubwa.

Aliandika: “Mwanangu, nani ambaye asingefurahia kuwa na mtoto kama wewe. Bravo, bravo, bravo.

“Wewe ni mfungaji halisi. Kila msimu umekuwa kwenye ubora wako, msimu uliopita mabao 22, msimu huu mabao 22. Nachoweza ni kukupongeza tu na kukwambia, najivutia. Lazima tufanye uamuzi sahihi katika kipindi hiki cha kumalizia maisha yako ya mpira.

“Wanazungumza sana kwenye vyombo vya habari, hawafahamu kwamba sisi ni Wabantu na kisha kuna mabosi ambao watalazimika kupata ushauri wa mtu mwenye busara ambaye ni baba yako.

“Tutalimaliza hilo punde, lala kwa amani mwanangu, baba yako anatazama kila kitu. Nakupenda.”

Arsenal wenyewe baada ya ushindi kwa Watford, walituma picha ya Aubameyang kwenye ukurasa wao wa Twitter, ikimwonyesha akishangilia moja ya mabao yake pamoja na emoji ya mkono unaoandika, jambo lililoibua matumaini kwamba huenda mchezaji huyo atakuwa amesaini dili jipya huko Emirates.