Baba, mchumba wamsindikiza Harmonize kutoa misaada Mbagala

Friday February 8 2019

 

By Nasra Abadallah na Hellen Hartle (DSJ)

Dar es Salaam. Msanii Rajabu Abdul maarufu kwa jina la Harmonize amepewa kampani na baba yake mzazi Mzee Abdul pamoja na mchumba wake wa kizungu Sara katika shughuli ya kutoa misaada mbalimbali kwa makundi yenye uhitaji maalum kama njia ya kushukuru.
Harmonize ambaye amezindua nyimbo nne kwa wakati mmoja (EP) amefanya hivyo ili kupata baraka za wakazi hao wa Mbagala kwani wamekuwa ni sehemu kubwa ya mashabiki wake.
Tukio hilo la uzinduzi limefanyika leo Ijumaa, Februari 8, 2019 katika viwanja vya Zakiem Mbagala jijini Dar es Salaam ambapo Harmonize alitoa vitu mbalimbali kama baiskeli kwa walemavu, unga, sabuni na fedha taslimu.
Akizungumza katika tukio hilo, Harmonize amesema ametoa msaada huo kwa lengo la kuwasaidia na kumshukuru Mungu kufanikisha kuachia nyimbo hizo na msanii maarufu kutoka
Nigeria, Bana Boy.
Amesema, katika EP hiyo yenye nyimbo nne, tatu ameimba na msanii huyo na moja akiwa amemshirikisha Naseeb Abdul 'Diamond'.
Kutokana na kufanikisha hilo amesema ana kila sababu ya kumshukuru Mungu na kufurahia na makundi hayo kwa kile kidogo alichojaliwa.
Mmoja wa wanufaika akiwemo, Mariam Hassan alishukuru kwa msaada huo na kumwombea Harmonize kuendelea kufanya vizuri.
Mwenyekiti Serikali ya Mtaa wa Mpakani Kata ya Mbagala, Salum Mahege, ambaye Mananchi wake 25, walipata msaada huo, amesema kitendo alichofanya msanii huyo, kinawapa wazazi
matumaini kwamba muziki sasa ni kazi kama zilivyo nyingine ambazo zinaweza kusaidia si watu wa familia ya mwanamuziki bali na wengine katika jamii.

Advertisement