BIGI: Mtanzania anakiwasha Australia, safari ya hispania inanukia

Tuesday June 2 2020

 

By ELIYA SOLOMON

WIKI chache zijazo, Dieudonne Bigirindavyi ambaye ni kinda la Kitanzania aliyepo nchini Australia, anaweza kukwea pipa na kwenda Hispania kuanza maisha yake mapya ya soka katika klabu ya AD Merida.

Yamkini kinda huyu ni mgeni machoni pako kutokana na kutocheza kabisa soka hapa nchini lakini tambua yakuwa ni Mtanzania kabisa na sio wa kuchakachua kutokana na wazazi wake wote wawili kuwa Watanzania.

Kama ambavyo tumekuwa mstari wa mbele kuwaibua na kukuletea maendeleo ya wachezaji mbalimbali wa Kitanzania kupitia gazeti hili, basi leo tunaye, Bigirindavyi ambaye alizaliwa huko mkoani Kigoma, Kaskazini Magharibi mwa Tanzania.

Akiwa Australia, Bigi mwenye miaka 18, anazungumzia vile ambavyo amepata nafasi ya kwenda Hispania kujiunga na AD Merida ambayo inashiriki Ligi Daraja la Pili ambayo ni maarufu kama Segunda División B.

Bigirindavyi anasema mchakato wa kupata shavu la kujiunga na AD Merida, ulitokana na kufanya kwake vizuri mwaka jana katika majaribio ya wiki kadhaa aliyoyafanya.

“Nilitakiwa kuwa Hispania kwa sasa lakini imeshindikana kwa sababu ya hili janga la virusi vya corona, itabidi nisubiri hadi hapo mambo yatakapokuwa sawa. Naendelea na mazoezi katika klabu yangu ya Brisbane City.

Advertisement

Nafasi ya kwenda kufanya majaribio katika hiyo timu, nilijiandaa vya kutosha ndio maana walinielewa na haikuchukua muda wakala wangu alinieleza kuwa amepokea taarifa kuwa AD Merida inanihitaji.

“Nilifurahi sana kwa sababu naamini hiyo ni nafasi kwangu ya kupiga hatua, ni timu ya daraja la chini Hispania lakini levo yake ya ushindani ni mkubwa ukilinganisha na hapa Australia.”

Kwa mujibu wa maelezo ya wakala wake, Bigi anasema AD Merida wanataka kuwa naye katika kikosi chao cha vijana kabla ya kuanza kumtumia kwenye kikosi chao cha kwanza ambacho kipo chini ya Juanma Berrero.

Kinda huyo, anasema aliondoka Tanzania na kwenda Australia akiwa mdogo na familia yake na huko ndipo alipoanzia maisha yake ya soka akiwa na umri wa miaka sita.

“Wazazi wangu wamekuwa wakinisapoti tangu nikiwa mdogo, kila hatua ambayo nimekuwa nikipiga ni ambao wapo nyuma yangu,” anasema Bigi ambaye amekuwa akicheza kama winga wa kushoto.

Katika vitu ambavyo Bigi anasema hawezi kuvisahau ni pamoja na majeraha ambayo aliyapata ya kuvunjika mguu na kumfanya akae nje ya uwanja kwa takribani miezi sita, “Kilikuwa kipindi kigumu sana kwangu katika uchezaji wangu mpira.

“Tulikuwa tukufanya kitu kama majaribio hivi wachezaji walikuwa wengi kutoka mitaani, kila mmoja alikuwa akiihitaji nafasi ya kuchukuliwa, kuna jamaa alinichezea vibaya ndo hapo nikabainikia kuwa nilivunjika,” anasema.

Pamoja na kuwa kwake Australia kwa miaka mingi, winga huyo, anasema amekuwa akizifahamu klabu za Simba na Yanga. “Najua kuwa ni wapinzani wakuu katika soka la Tanzania, nimekuwa nikiona mengi katika mitandao ya kijamii.

“Watanzania wengi wanaonekana kupenda sana mpira ndio maana pengine Simba na Yanga zimekuwa na wafuasi wengi,” anasema.

Australia ambako yupo Bigi kuna klabu mbalimbali zenye uhasama, ikiwemo kati ya Sydney FC dhidi ya Western Sydney Wanders, nyingine ni kati ya Melbourne Victory dhidi ya Melbourne City.

Katika mahojiano yetu, Bigi amemtaja mshambuliaji wa zamani wa Chelsea, Didier Drogba kuwa ndiye mchezaji aliyemfanya kulipenda soka pamoja na kuwa amekuwa akivutiwa pia na staa wa klabu ya Juventus, Cristiano Ronaldo.

“Nimekuwa nikipenda kumtazama Drogba hadi leo pamoja na kwamba kati ya Messi na Ronaldo huwa nampenda Ronaldo. Huwa navutiwa na matumizi mazuri kati ya akili na nguvu za Drogba, mabeki waliipata,” anasema.

Advertisement