BARES : Mabosi wa Prisons hawakutaka niondoke

Muktasari:

  • Katika mahojiano maalumu yaliyofanywa na Mwanaspoti nyumbani kwao Unguja mtaa wa Kandanda, Bares alielezea mambo mbalimbali aliyokutana nayo.

MIONGONI mwa makocha waliofanya vizuri katika Ligi Kuu Bara wakitokea Zanzibar basi ni Mohamed Abdallah ‘Bares’ ukiachana na akina Malale Hamsini, na Ahmed Morocco ambao wamewahi kuitumikia timu ya Taifa ‘Taifa Stars akiwa kama Kocha Msaidizi.

Bares akiwa Bara alianza kuifundisha Ndanda FC na baadaye Prisons walimchukua timu yao ikiwa katika hali mbaya ya kutaka kushuka daraja msimu uliopita.

Kocha huyo alipigana kuhakikisha timu inabaki kwenye ligi, hilo alifanikiwa na yeye kuibuka kocha bora wa msimu uliopita.

Msimu huu mambo yalikuwa magumu kwake kwani alianza vibaya jambo ambalo lilipelekea kuvunjwa kwa mkataba wake huku viongozi wa Prisons wakiamua kuondoa watu wote kwenye benchi la ufundi pamoja na uongozi wa timu wote.

Katika mahojiano maalumu yaliyofanywa na Mwanaspoti nyumbani kwao Unguja mtaa wa Kandanda, Bares alielezea mambo mbalimbali aliyokutana nayo.

Msimu uliopita

Anasema alipoingia Prisons alikuwa na mambo machache ya kufanya ili timu ibaki kwenye ligi,

“Kikubwa ilikuwa ni kuitengeneza timu kisaikolojia, hatukutaka ubingwa zaidi tu ya kubaki kwenye ligi, kwasababu timu ilikuwa na wachezaji wazuri kwa wakati, ule hivyo ilikuwa ni kazi rahisi tu ya kufanya ili ikae vizuri.

“Hili liliwezekana kila mmoja alicheza kwa kujiamini hawakuwa tena na hali ya kuhofia kushuka daraja, walijiamini kwamba wanaweza kuondoka kwenye hatari,” alisema.

Msimu huu

Ulikuwa ni msimu mbaya kwake ambapo anaelezea sababu za kuboronga kwake,

“Kwanza tulistahili vibaya baada ya wachezaji wetu waliotusaidia msimu uliopita kuondoka, waliopo hawana uwezo mkubwa hata viongozi wanaijua hilo kwamba timu ya sasa ni tofauti na msimu uliopita, haya matokeo kila mmoja aliyatarajia.

“Ukitaka kulifahamu kitu vizuri uzuri na ubaya wake ni lazima ukifanye mwenyewe, ndivyo ilivyo hata Prisons nilipoingia ilikuwa tofauti na nilivyokuwa naiona ila sitaki kuzungumzia mengi yaliyomo ndani ya timu hiyo.

“Kwenye usajili nilipendekeza wachezaji, lakini waliowengi hatukupata kwasababu ya hali ya uchumi, mabosi unawapelekea mapendekezo lakini unaambiwa hakuna pesa hivyo linakuwa jambo gumu kidogo kutekeleza kile ulichokusudia na unalazimika kusajili wale wanaolingana na hali ya uchumi kwa wakati huo.

“Wakati wanafanya maamuzi yao ya kuwaondoa viongozi wao walitaka mimi nibaki kwenye timu, nilikataa kwasababu ni jambo ambalo haliwezekani, wale niliokuwa nafanyanao kazi waondoke nibaki mimi ingeleta picha mbaya ndipo tulipokubaliana kwamba tuvunje mkataba ili waanze upya ila kiukweli wao hawakutaka niondoke,” anaeleza.

Timu 16 zinatosha

Bares anasema kutokana na kukosa mdhamini ingefaa kuwepo na timu 16 kama mwanzo na sio 20 za sasa.

“Kwanza ingesaidia kupunguza gharama kwa timu, kwani uwepo wa timu 20 umeongeza gharama kubwa wakati hakuna udhamini.

“Timu ambazo uchumi wao mdogo zinaumia na zinashindwa kumudu gharama za safari nyingi kutokana na uchumi wao mdogo, mbaya zaidi ukiwa mgeni huambulii kitu chochote hilo walipaswa waliangalie kwa mapana zaidi, haiwi bora kwani ushindani unakuwa mdogo.

“Pia ingepunguza kuwepo na mizozo isiyokuwa na maana kwasababu timu ikishindwa kusafiri lazima mzozo uibuke na hata mishahara kwa wachezaji inakuwa ya shida kwasababu viongozi wa klabu wanakuwa na mambo mengi ya kufanya yanayotumia pesa nyingi, ikiwemo kusafirisha timu kwenda sehemu nyingi.

Ratiba

Bares anaelezea juu ya ratiba ya ligi “ratiba haiki vizuri kwasbabau kila mara inabadilika na wakati mwingine inabadilika wakati timu inaelekea kucheza mechi ya ugenini hivyo gharama za kukaa ugenini zinaongezeka hilo pia waliangalia wanaosimamia,”

Kwanini anaitwa Bares

Anasema hakujiita hilo jina, “Wakati nacheza mashabiki ndiyo walionipa jina la ‘Bares’ wakinifananisha na mchezaji wa Italia anayeitwa Franco Baresi hivyo lilizoeleka hadi sasa.

“Tangu mcheza timu ya Black Sela na New Stars ambapo nilicheza nafasi mbili beki na kiungo hapo ilikuwa ni timu ya Ligi Kuu,”

Furaha na huzuni yake

Bares ambaye ni baba wa familia ya watoto wanne anaelezea:

“Moja ya mafanikio ambayo nimeyapata kupitia soka ndani ya miaka 22 ya kucheza na kufundisha ni umaarufu ambao sasa naweza kuingia popote ni kusaidiwa jambo langu hilo ndilo kubwa katika maisha yangu.

“Niliacha kucheza ili nifundishe kwasababu ndiyo kitu nilichokuwa nakipenda kuliko hata kucheza, na kipindi nacheza nilifanya kazi mbili kwamaana ya kuwa kocha mchezaji ingawa baadaye niliamua kuachana na kucheza ili nifanye kile ninachokipenda.

“Ila hakuna jambo gumu nililokutana nalo kwenye soka zaidi ya kupokea taarifa za vifo viwili vya watu wangu wa karibu ambazo nilizipata nikiwa kwenye mechi, kifo cha kocha Jumanne Tambwe na baba mkwe wangu, nilipata wakati mgumu hata kusimamia timu,”

Kujiandaa kutimuliwa

Bares anasema mtu yoyote anapokuwa kiongozi sehemu ama kocha basi akubaliane kwamba muda wowote anaweza kuondolewa kwenye nafasi hiyo.

“kuondolewa ni jambo la kawaida katika mpira ingawa pia unaweza kuamua kuondoka mwenyewe, hivyo vyote viwili vinaweza kutokea, kufukuzwa ama kuondoka mwenyewe inategemea na sababu husika.

“Wengi wanasema wanawaondoa makocha kwa sababu ya uwezo wao mdogo ila hilo sio kweli, kuna sababu nyingi za kufikia maamuzi hayo, ila sio viwango tu, kuna mengi sana yamejificha nyuma ya makocha kufukuzwa au kuvunja mkataba,”

Anaeleza viongozi wengi wanapenda kuona timu zao zikifanya vyema lakini kuwajibika kwenye nafasi zao kunakuwa na ugumu na hapo ndipo matatizo mengi yanapoanzia.

Itaendelea kesho Jumanne.