BARBARA: Nataka Simba iwe Zamalek

USIJIDANGANYE kabisa juu ya muonekano wake na wala usimchukulie poa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez. Boss Lady huyo ni mwanamke wa shoka na ukipitia wasifu wake katika utendaji na mikakati aliyonayo ni wazi Simba imelamba turufu.

CEO huyo mwenye umri wa miaka 30, ameingia katika kitabu cha historia nchini kwa kuwa mwanamke wa kwanza kushika nafasi hiyo katika ngazi ya klabu, lakini akiingia kwenye historia ya wanawake waliowahi kushika vyeo vya juu kwenye sekta ya michezo akifuata nyayo za Lina Madina Mhando aliyewahi kuwa mwenyekiti wa Chama cha Soka la Wanawake Tanzania (TWFA) na Rais wa Shirikisho la Ngumi Tanzania (BFT), Joan Minja miaka kadhaa iliyopita.

Mwanaspoti limefanya mahojiano maalumu na Barbara ambaye amefunguka mambo kadhaa baada ya kuanza majukumu yake tangu ateuliwe na kutangazwa wiki iliyopita na Ceo huyo mpya wa Simba ameanika mikakati yake na ndoto zake za kutaka kuipaisha Simba kimataifa.

Anasema kwa kushirikiana na viongozi wenzake na Wanasimba kwa ujumla, anaamini Simba itakuja kuwa kama Zamalek ama klabu nyingine kubwa za Afrika Kaskazini. Kivipi?

Endelea naye upate utamu wa namna Barbara alivyo na ndoto za kuifanya Simba iwe ya kimataifa zaidi baada ya kutamba na rekodi zake katika soka la ndani.

MTU WA KAZI

Barbara anasema siri ya mafanikio katika utendaji kazi zake ni kuwa ‘siriazi’ na sio mtu wa mchezomchezo kama watu wanavyomchukulia.

Anasema nguzo yake kubwa ni kufanya kazi kwa weledi, kujali muda na kuleta ufanisi hata kama ni kwa muda mfupi. Mbali ya kushika nafasi za juu, Barbara pia ameweka historia ya kuwa kiongozi wa kwanza mwenye umri mdogo kushika madaraka hayo kwa klabu hiyo kongwe nchini.

Anasema siri kubwa ya kuingia katika soka ni malengo yake wakati akiwa mdogo kuwa anapenda kufanya kazi za jamii.

“Napenda kutumikia jamii, hii ndiyo ilikuwa ndoto yangu tangu nilipokuwa mtoto. Niliweka nadhiri hiyo, nina uwezo wa kufanya kazi nyingine kama benki na kampuni nyingine kutokana na weledi wangu,” anasema Barbara na kuongeza:

“Mpaka sasa nimeweza kufanya kazi kwenye taasisi mbalimbali za kimataifa nikifanya kazi nyingine. Hata hivyo, bado nilikuwa na ndoto ya kufanya kazi kwa ajili ya kuitumikia jamii.”

MO DEWJI AMPA ULAJI

Barbara aliyezaliwa mwaka 1990 jijini Dar es Salaam kwa baba Mcolombia na mama Mtanzania, anasema baada ya kufanya kazi na kampuni ya Deloitte, aliwaambia wazazi wake kuhusiana na malengo yake ya kufanya kazi kwenye mashirika ya kijamii zaidi ndipo akapata kazi kwenye taasisi ya Mohammed Dewji Foundation.

“Nilianza kuona mwanga kwa kile nilichokipanga ndani ya maisha yangu. Nilifanya kazi kwa juhudi na weledi wa hali ya juu mpaka kufikia bosi wangu (Mo) kunipandisha cheo na kuwa mkuu wa wafanyakazi wa taasisi hiyo,” anasema Barbara na kuongeza:

“Naweza kusema kazi ya kuwa CEO wa Simba haikuwa moja ya malengo yake katika maisha. Ila kutokana na hali ilivyokuwa wakati nikiwa nafanya kazi za Mo Foundation, nilipata mwanya wa kujua kuhusiana na kazi hiyo na hasa baada ya kuingia kwenye mfumo wa klabu.”

Anasema aliweza kufanya kazi nyingi za Simba huku akiwa na majukumu yake kwa Taasisi ya Mo na kupata wasaa wa kujifunza masuala ya soka na kuweza kupanua wigo na uzoefu wake.

“Mimi sijawahi kuwaza kuwa kocha au kiongozi wa soka pamoja na kujua masuala mbalimbali, kwa kifupi, kufanya kazi za Simba ilikuwa kama elimu kwangu,” anasisitiza.

NDANI YA SIMBA

Barbara anasema aliendelea kujifunza mambo mbalimbali ambayo yanahusiana na soka kupitia vikao vya bodi ya wakurugenzi na vinginevyo.

Anasema kufanya kazi na watu kama Mulamu Nghambi, Crescentius Magori, Asha Baraka, Abdallah Salim ‘Try Again’ na wengine kibao lilikuwa ni darasa kubwa sana kwake.

Anasema kutokana na hali ilivyokuwa alijikuta akifanya maandiko mengi ya klabu na yale ambayo yalikuwa yanahusu kazi za mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi.

“Niligundua kazi za klabu ya Simba ni sawa na kazi nyingine ambazo nilifanya nikiwa kwenye mashirika mbalimbali ya kimataifa,” anasema.

Anasema kutokana na hilo, hakuwa na presha ya kazi zaidi ya kuongeza ufanisi ambao wakati Senzo anaondoka, hawakuwa na mshtuko kwani kazi zake ziliweza kufanyika.

Anaongeza kuwa, kutokana na majukumu ya kila mfanyakazi na juhudi zake katika kufanya kazi, aliteuliwa kushika nafasi hiyo baada kwa kupata ridhaa kutoka kwa wajumbe wote wa bodi ya wakurugenzi.

SIMBA KAMA ZAMALEK

Kama ilivyokuwa kwa viongozi wengine, Barbara ameweka mipango kadhaa ya kuiendeleza klabu hiyo ili kufikia maendeleo ya juu kabisa.

Moja wa mipango mkakati ni jinsi gani ya kuongeza mapato kwa ajili ya timu ya wanaume na wanawake, Simba Queens, na hatimaye kujitegemea katika masuala mbalimbali ya kimichezo.

Anasema mpango mkubwa ni kuongeza wanachama na kuwezesha kupata mapato kupitia kadi za uanachama. “Pia kuna mpango wa kuuza bidhaa mbalimbali zenye nembo ya timu na kuwapa wanachama na mashabiki chaguo la manunuzi mbali ya jezi.”

Anasema kuna watu wanapenda kuvaa jezi, wapo wanaotaka kuvaa fulana za kawaida, kuwa na vishikio vya funguo, tracksuit, mavazi ya kawaida na vitu vingine kemkem.

Mbali ya hivyo, pia Barbara anasema anataka kuongeza thamani ya klabu hiyo kufikia timu kubwa za Afrika kama Zamalek, Al Ahly na nyinginezo ambazo zinaweza kumnunua mchezaji kwa Sh1 bilioni na kuendelea.

Anasema kwa soka la ndani Simba wameziacha mbali klabu nyingine kwa kuwa na timu bora yenye kuundwa na wachezaji wenye vipaji wa ndani na nje ya nchi, lakini umefika wakati sasa kufunika anga la kimataifa ili kuanza kuvuna fedha za wadhamini wa michuano ya CAF.

Anasema ili kula sahani moja ama kulingana na klabu kama Zamalek ni lazima timu iwe na wachezaji wenye viwango vya juu ambao usajili wao una dau kubwa, na klabu kama haina fedha za kutosha ni ngumu.

“Kufika huko kunahitaji mipango mikubwa na kuungwa mkono na wanachama. Kwa mfano, kama Simba itaongeza wanachama wake ikafikia hata wawe milioni 10 na kila mmoja akilipa ada kwa wakati, timu itaingiza mabilioni ya fedha na kumudu kununua mchezaji hata kwa Sh1 bilioni,” anasema Barbara.

“Kama klabu itakuwa inaingiza fedha za kutosha, kwanini isiweze kumsajili mchezaji wa gharama kubwa ambao wataweza kuleta matokeo chanja ndani ya timu? Zamalek, TP Mazembe na klabu nyingine zinazotamba Afrika zimefika huko kwa vile zina uchumi mkubwa, kitu ambacho Simba ikikazana inaweza kufika huko na kutikisa Afrika.”

Anafananua zaidi kwa kusema: “Kuna kampuni kubwa duniani zinazofanya biashara, mpaka sasa hawajafikia kupata wateja milioni 35, lakini wanaendesha biashara zao vizuri na kwa faida kubwa, lengo langu ni kuona Simba inafikia huko hata kwa nusu yake.” Anasema fedha ndio mpango mzima wa kufikia malengo kwa timu na kuna mipango inayofanyiwa kazi ili kuona wapi wanafika.

“Nimeshiriki katika miradi mingi sana, mfano mpango mkakati wa kuirejesha kwa nguvu zote Air Tanzania Limited (ATCL) na mpaka sasa kuna maendeleo makubwa, kwa mapenzi ya Mungu, naamini tutafanikiwa,” anasema.

Anafafanua kuwa Simba ni taasisi yenye mafanikio makubwa katika soka na jina linatakiwa kwenda na thamani ambayo ndiyo kazi kubwa ya uongozi.

Mtendaji huyo anasema pamoja na ukubwa wake, bado kuna changamoto za kupata wanachama wa kutosha wa kulipia ada na kuchangia maendeleo. “Nimeweka mpango mkakati wa kuongeza wanachama na kufikia idadi ambayo inafanana na ile ya wanachama wanaohudhuria mechi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa. Kwa mfano, Simba Day iliingiza watazamaji wengi sana na kupata mamilioni ya fedha. Je klabu itashindwaje kuongeza idadi ya wanachama ambao wanalipia kiingilio kuona mechi za timu yao kuwa mwanachama wa klabu?” anahoji Barbara.

“Ni ukweli usiopingika kuwa wanachama wanaofika uwanjani kuona mechi wanazidi idadi ya wanachama ambao wapo kwenye leja ya klabu. Lengo ni kutoka hapo na kuongeza idadi ya wanachama na kujiongezea kipato kila mwezi, miezi sita au mpaka mwaka.”

Pia anasema ili kuwahamasisha wanachama kuchangia timu yao, watahakikisha timu yao ina shinda mechi na kuendelea kutawala soka la Tanzania pamoja na mkakati wao mkubwa wa kufanya vyema katika mshindano ya kimataifa.

“Nawaomba mashabiki wa simba kuendelea kuisapoti timu yao na wale ambao si wanachama, nawaomba wafanye hivyo.”