Azam yatangaza kufukuzia ubingwa Ligi Kuu

Muktasari:

Azam wana kumbukumbu  ya kupoteza mchezo mmoja wa Ligi Kuu Tanzania Bara ambapo ilikuwa mbele ya Mtibwa Sugar, Desemba 29 mwaka jana kwa mabao 2-0.

Dar es Salaam. Kocha wa Azam FC, Hans van der Pluijm amesema mkakati wake ni kutopoteza tena  mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara  ili kujiweka kwenye mazingira mazuri  ya kutwaa ubingwa wa ligi hiyo.
Azam wana kumbukumbu  ya kupoteza mchezo mmoja wa Ligi Kuu Tanzania Bara ambapo ilikuwa mbele ya Mtibwa Sugar, Desemba 29 mwaka jana kwa mabao 2-0.
Pluijm alisema kipigo chao cha kwanza cha msimu huu  kwenye Ligi dhidi ya Mtibwa  kimemfanya awe makini na mbinu zake mbalimbali ambazo amekuwa akizitumia ili kuendelea kusalia kwenye mbio za ubingwa.
“Bado tuna nafasi ya kuchukua ubingwa na siku zote mpira umekuwa mchezo wa makosa, tulikosea ndio maana Mtibwa walitufunga lakini kutufunga kwao kuliacha somo kwetu.
“Nina kikosi chenye uwezo wa kupambana, hilo ni jambo la kujivunia kwa hiyo sitegemei kuendelea kupoteza pointi kama tutashindwa kushindi ni bora tubaki na alama moja kuliko kupoteza.
“Inaumiza kupoteza wakati wapinzani wako wanashinda, sina presha nao kabisa  kwa sababu najua nitakutana nao na michezo dhidi yao naamini itakuwa na nafasi kubwa ya kuweka utofauti wa pointi,” alisema kocha huyo wa zamani wa Yanga na Singida United.
Azam ipo nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara wakiwa na pointi 44  walizozikusanya kwenye michezo 19, vinara wa ligi hiyo, Yanga wanaongoza wakiwa na alama 53 huku wakina mchezo mmoja mbele.