Azam yasajili Kisu kingine

Kipa wa zamani wa Singida United na Gor Mahia, David Kisu amesaini mkataba wa miaka miwili na Azam FC. Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin 'Popat' alisema kuwa wameamua kuongeza nguvu kwa upande wa makipa baada ya kuachana na kipa Mghana, Razak Abalora.

Alisema kuwa wanafanya usajili kwa umakini zaidi ili kufanya vyema katika msimu ujao.

"Bado tunaendelea na usajili ambao kocha amependekeza, lakini pia tutapandisha wachezaji chipukizi wenye uwezo mkubwa, tumekwisha mpandisha kipa wa timu ya watoto ambaye sasa anafanya mazoezi na timu ya wakubwa," alisema.

Alisema wanataka kutwaa ubingwa msimu ujao na ndiyo maana wameanza mazoezi mapema.

Azam tayari imeanza mazoezi na mastaa wake wapya,kama Ally Niyonzima, Awesu Awesu na Ismail Azizi.

Ligi Kuu ya Bara msimu ujao inatarajiwa kuanza Septemba 6 kwenye viwanja mbalimbali nchini.

Simba ndiyo waliotwaa ubingwa msimu uliopita huku Yanga wakiwa wa pili.

Kwa habari kamili za usajili endelea kufuatilia mitandao yetu ya kijamii pamoja Gazeti la Mwanaspoti kesho Ijumaa Agosti 7, 2020.