Azam yapania kulipa kisasi kwa Simba

Monday May 13 2019

 

By Imani Makongoro

Dar es Salaam. Wakati mashabiki wa Simba wakihesabu saa kuona kama watapooza machungu ya kipigo cha Kagera Sugar, kocha wa Azam, Abdul Mingange amesema anafahamu udhaifu wa Simba na atautumia kupata pointi watakapokutana Leo.

Simba na Azam watacheza Leo kwenye uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam mechi ya mzunguko wa pili baada ya ile ya mzunguko wa kwanza Azam kulala kwa mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Taifa.

Akizungumzia mchezo huo, Mingange amesema ni wa kulipa kisasi na bahati nzuri anafahamu udhaifu wa Simba uko sehemu gani kuelekea kwenye mchezo huo.

“Tunahitaji kulipa kisasi, mbinu gani nitatumia mashabiki wataokuja uwanjani wataona,” alisisitiza Mingange.

Alisema Simba ina kikosi kizuri, inaongoza Ligi, wana kocha mzuri, ina uchumi mzuri na wametoka kushiriki mashindano ya kimataifa na kufanya vizuri, lakini hivyo si vigezo vya kuwanyima pointi Azam.

“Pamoja na vitu hivyo, lakini bado wana tatizo la uchovu, siyo Simba ile ya mwanzo, wachezaji watakuwa wamechoka kwa kucheza mfululizo, hivyo hawatupi presha,” alisisitiza Mingange.

Advertisement

Alisema anafahamu mechi itakuwa ngumu kwa sababu timu zote ni kubwa, lakini mpango wa Azam ni kulipa kisasi.

Akizungumzia mpango wao kumaliza Ligi kwenye nafasi za juu, Mingange alisema katika harakati za ubingwa na nafasi ya pili wamejitoa na kuwachia vigogo wa Soka nchini, Simba na Yanga.

Advertisement