Azam haiachi kitu, Cheche afunguka mazito Chamazi

Muktasari:

Akizungumza baada ya mchezo wa juzi mjini Shinyanga, Cheche alisema licha ya vijana wake kupambana na kupata pointi tatu, lakini bado tatizo la umaliziaji mipira ya mwisho linawatesa.


HIYO Azam FC msiichukulie poa kwani kasi yake kwenye Ligi Kuu inaendelea kutikisa baada ya juzi kuichapa Mwadui FC bao 1-0, huku Kocha Msaidizi Idd Cheche akitamka kwamba bado washambuliaji wao wanawaumiza kichwa.

Ushindi wa juzi ulifikisha mechi tano mfululizo kwa kikosi hicho bila kupoteza mechi hata moja, ikiwa awali walianza na Polisi Tanzania 1-0, ikaichapa Singida 2-1, ikailaza Lipuli 2-0, Yanga akafa 1-0 na Mwadui 1-0.

Kutokana na ushindi huo, timu hiyo inafikisha pointi 35 na kukaa nafasi ya pili baada ya kucheza mechi 16, huku ikizidiwa alama sita na vinara wa Ligi Kuu Simba waliocheza idadi sawa ya michezo.

Akizungumza baada ya mchezo wa juzi mjini Shinyanga, Cheche alisema licha ya vijana wake kupambana na kupata pointi tatu, lakini bado tatizo la umaliziaji mipira ya mwisho linawatesa.

Alisema benchi la ufundi litaendelea kulifanyia kazi tatizo hilo ili katika mechi zinazofuata waweze kuvuna idadi kubwa ya mabao na kuendelea kujiweka pazuri kwenye msimamo.

“Tunashukuru kwa ushindi licha ya kupata ushindani mkali, lakini bado tunapoteza nafasi nyingi za wazi kwahiyo tunaenda kujipanga upya na kusahihisha makosa ili mechi zijazo tufanye vizuri,” alisema Cheche.

Kocha huyo aliongeza kuwa baada ya mchezo huo, kwa sasa kikosi kinarudi Dar es Salaam kujipanga tena kwa ajili ya mchezo wao wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Friends Rangers.

“Mechi inayofuata ni dhidi ya Friends Rangers ya Kombe la Shirikisho, tunaenda kujiandaa kuhakikisha tunashinda na kusonga mbele, sisi kila mchezo ni vita ya ushindi,” alisema.