Azam FC wala haina presha

LICHA ya kupata sare ya kwanza sambamba na kutoka kupokea kipigo kimoja kwenye Ligi kuu, nyota wa Azam FC wametamba hawana presha kwa vile lengo lao ni kuona msimu huu wanabeba ndoo.

Akizungumza na Mwanaspoti, Nahodha Msaidizi wa Azam FC, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ alisema kupoteza pointi tano si tatizo kubwa kwao, licha ya ukweli soka ndivyo lilivyo, lakini bado wanajipanga kwa vile ligi ni mbichi na watapambana ili kuona wanatimiza ndoto zao.

Sure Boy, ambaye ni mchezaji mwandamizi wa matajiri hao wa Kibongo alisema kila wanapokutana na Mtibwa Sugar, hupata tabu mbele ya wapinzani hao, ingawa mipango yao ilikuwa kupata ushindi ili kuendeleza rekodi ya kushinda mechi mfululizo.

“Uzuri ni kwamba ligi ndio kwanza ipo mwanzo kwa mechi zilizobaki tunajipanga kupata matokeo mazuri kwa kuamini makocha wetu wameona makosa na watayarekebisha, bado tuna nafasi ya kurudi kwenye mstari tulioanza nao,” alisema Sure Boy aliyefunga bao la kusawazisha dhidi ya JKT Tanzania.

Azam iliyocheza mechi tisa na kukusaka alama 22 kama ilizonazo Yanga, inasaka taji lao la pili la Ligi Kuu kwani tangu ilipotwaa kwa mara ya kwanza msimu wa 2013-2014 imekuwa ikiambulia patupu mbele ya vigogo Simba na Yanga zinazopokezana taji hilo tangu wakati huo.