Azam FC: Nafasi ya tatu Ligi Kuu ni yetu

Muktasari:

Simba ya Kocha Patrick Aussems ndio inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 81, mbele ya Yanga inayoshika nafasi ya pili na pointi 80 na Azam FC ni ya tatu wana pointi 68. Simba wamebakiwa na mechi sita mkononi wakati Yanga na Azam FC wana mitatu kila mmoja.

Dar es Salaam. Mipango ya Kocha wa Azam FC, Meja Abdul Mingange ni kumaliza Ligi Kuu akiwa kwenye nafasi ya pili imegonga mwamba na sasa matajiri hao wa Chamazi wamejihakikishia nafasi ya tatu msimu huu.
Azam FC ambayo imesalia na michezo mitatu sawa na Yanga baada ya kucheza mechi 35 katika ligi yenye timu 20, wanashika nafasi ya tatu na pointi 68, Yanga ya pili yenye michezo 35 pia ni wa pili na pointi 80 wakati Simba wao ndiyo vinara wana pointi 81 na wamecheza mechi 32.
Kwa sasa Yanga wana nafasi kubwa ya kumaliza katika nafasi hiyo ingawa Kocha Mwinyi Zahera anaendelea kupigia mahesabu ubingwa wa Ligi Kuu.
"Bado nafikiria kumaliza Ligi Kuu katika nafasi ya pili, sisi (Azam) kama tukishinda mechi zetu zote, lolote linaweza kutokea. Kikubwa ni kushinda mechi zote zilizobaki," alikaririwa Mingange.
Azam yenye pointi 68, ikishinda michezo yake yote mitatu iliyosalia itafikisha pointi 77 ambazo zinamhakikishia nafasi ya tatu kwani timu 17 za chini kwenye msimamo, hata zikishinda mechi zao zote haziwezi kuishusha Azam FC.
Mbali na Azam kujihakikishia nafasi ya tatu, Klabu ya African Lyon inayomilikiwa na Rahim Zamunda tayari imeshuka daraja licha ya kuwa na michezo minne mkononi.
African Lyon ina pointi 22 ikishinda michezo yote minne itafikisha pointi 36, ambapo sasa itasubiri timu nyingine zinazoning'inia kwenye msimamo kati ya Mwadui FC (pointi 37), JKT Tanzania, Biashara United na Mbeya City zenye pointi 40 na Coastal Union, Stand United na Alliance zenye pointi 41 kila moja.