Aussems athibitisha kuvunja mkataba Simba

Muktasari:

Miongoni mwa tatizo lililomuondoa kikosi kocha huyo ambaye aliifikisha Simba hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita ni kuondoka nchini bila kufuata taratibu za ruhusa kwa waajiri wake.

LEO Jumamosi mchana, uongozi wa Klabu ya Simba umevunja mkataba rasmi na kocha wao Patrick Aussems raia wa Ubelgiji.
Ni wiki mbili sasa tangu tetesi za kuondolewa kwa kocha huyo ziwepo, huku wakikaa vikao kadhaa kumjadili juu ya hatima yake ikiwemo kumuita kujieleza kalba ya kufanya uamuzi wa mwisho baada ya Kamati ya Nidhamu nayo kujadili.
Miongoni mwa tatizo lililomuondoa kikosi kocha huyo ambaye aliifikisha Simba hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita ni kuondoka nchini bila kufuata taratibu za ruhusa kwa waajiri wake.
Juzi Alhamisi, uongozi chini ya Mtendaji Mkuu Senzo Mazingiza uliitisha kikao ambacho Aussems alihudhuria ili kujieleza lakini maswali yote aliyoulizwa ilidaiwa alishindwa kuyatolea ufafanuzi ikiwemo kwanini aliondoka pasipo kufuata utaratibu, alikwenda wapi na kufanya nini.
Mchana wa leo, Aussems alifika kwenye ofisi za Mkurugenzi Mtendaji zilizopo Posta jijini Dar es Salaam kuitikia wito wa jana Ijumaa baada ya kamati ya nidhamu kujiridhisha na majadiliano yao, hivyo ilibaki kumkabidhi barua ya kuvunja mkataba wake ambao ulipaswa kumalizika mwishoni mwa msimu.
MCL Digital, lilizungumza na Aussems ambapo alikiri kupokea barua ya kuvunja mkataba wake.
"Klabu imenifukuza kazi rasmi kuanzia leo, kwasasa sio kocha wa Simba," alisema Aussems kwa ufupi na kukata simu.
Kwa habari zaidi na kwa kina usiache kusoma gazeti la Mwanaspoti na Mwananchi kesho Jumapili