Aussems ashindwa kujizuia

Muktasari:

Nyota Simba wamepewa mapumziko ya siku mbili na wanatarajia kuingia kambini Jumatatu tayari kwaajili ya maandalizi ya michezo ya ligi iliyombele yao.

WAKATI wadau wengi wakiendelea kujiuliza sababu za Kocha mkuu wa klabu ya Simba, Patrick Aussems kushindwa kuwatumia Miraji Athumani na Mzamiru Yassin katika mchezo wa ligi kuu dhidi ya Tanzania Prisons, kocha ameshindwa kujizuia na kufafanua sababu ya kuwachunia.
Kwenye mchezo huo uliopigwa katika uwanja wa taifa, Simba ililazimishwa sare ya kutofungana na Tanzania Prisons, ambapo baada ya mchezo mashabiki wa Simba walionekana kulalamikia juu ya sababu za kutowapanga wachezaji hao.
Akizungumza na Mwanaspoti, Aussems alisema alimpumzisha Mzamiru Yassin baada ya Jonas Mkude kurejea kikosi cha kwanza na ambaye anaimudu vizuri namba hiyo, huku akitaja sababu ya kutompanga Miraji ni kutokana na majeraha.
"Mashabiki wanaongea sana bila kufahamu sababu ni nini bado tuna michezo mingine mingi hao wachezaji wanaowataka watatumika sana, unajua Miraji aliumia hivyo asingeweza kucheza kama ilivyo kwa Bocco na Da Silva," alisema Aussems.
"Napanga kikosi kutokana na ubora wa mchezaji mazoezini sijawahi kukurupuka tumepoteza mchezo tuna nafasi nyingine ya kujipanga, Mzamiru hakucheza kwa sababu Jonas Mkude amerudi na tulimbadilisha kwa sababu amecheza mechi zote hizo tano," alisema.
Pia kocha Aussems ametoa siku 2 za mapumziko kwa wachezaji wake, ambapo watarejea Jumatatu, Novemba 11 tayari kujiandaa na mchezo unaofuata wa ligi utakaopigwa Novemba 24, baada ya mapumziko kupisha michezo ya kalenda ya FIFA.