Aussems alikubali gwaride la maafande

Friday November 8 2019

 

By Thobias Sebastian

MATOKEO ya suluhu katika mchezo wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara Simba dhidi ya Tanzania Prisons, yamemuibua kocha Patrick Aussems na kueleza tangu amefika nchini hajawahi kukutana na timu bora kama hiyo.
Aussems alisema tangu amekuja hapa nchini amekutana na timu nyingi lakini Tanzania Prison ni timu bora ambayo inacheza kwa nidhamu kubwa tena ndani ya maelekezo ambayo kila mchezaji alifanikiwa kuyatimiza majukumu yake.
"Ukiangalia aina ya uchezaji wa Prison waliingia wakiwa na maelekezo ya kuzuia na kushambulia kwa kushtukiza jambo ambalo kiukweli kila mchezaji wao alitimiza jukumu yake ipasavyo kwani tulishindwa kuwazidi na kupenya katika mianya ambayo waliiacha wazi kwa muda mchache," alisema.
"Aina ya uchezaji tu ambayo walikuja nayo Prison kwamba walikuwa wanataka kutuzuia muda wote na tulifanikiwa kutengeneza nafasi ambazo kama tungekuwa makini tungeweza kufunga bao lakini lilishindikana hilo.
"Niwapongeze Prison waliingia kwa mapango na nidhamu kubwa dhidi yetu ambayo kiukweli walifanikiwa kila mmoja kuifanya majukumu yake uwanjani na hii imekuwa timu yenye mbinu bora ya kuzuia kwangu tangu nimeanza kufanya kazi hapa Tanzania," alisema.
"Matokeo ambayo tumeyapata hayakunishangaza kwani tulifahamu tunakwenda kucheza na timu ambayo haijapoteza mchezo wowte mpaka sasa katika ligi," alisema Aussems ambaye aliongoza Simba kutwaa ubingwa wa ligi msimu uliopita na kufika katika hatua ya robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika.

Advertisement