Aussems Atua na mzuka

Muktasari:

  • Simba ina pointi sita, AS Vita na Al Ahly wana pointi saba wakati JS Saoura inaongoza kundi hilo ikiwa na pointi nane.

KOCHA wa Simba Patrick Aussems katua na mzuka mwanangu. Amesema mashabiki wa Simba wasihuzunike wala kuwa na wasiwasi, Jumamosi watafurahi wenyewe, robo fainali kwao, njia nyeupe kabisa.

Simba iliwasili jana saa 10 jioni ikitokea Algeria kwenye mchezo wa Kundi D wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya JS Saoura waliochapwa mabao 2-0 ikiwa ni kisasi baada ya awali Simba kuichapa timu hiyo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam,

Matokeo hao yameifanya Simba kushuka hadi nafasi ya mwisho kwenye msimamo wa kundi hilo kwa mara ya kwanza kwani ilikuwa ikichezea nafasi ya kwanza, pili na tatu.

Simba ina pointi sita, AS Vita na Al Ahly wana pointi saba wakati JS Saoura inaongoza kundi hilo ikiwa na pointi nane.

Hata hivyo, Kocha Aussems anajua mashabiki wa timu hiyo wana hasira za kufungwa, lakini akawatoa hasira na presha kwa kuwaambia wanaingia robo fainali bila utata wowote, kwani ni lazima wapinzani wao AS Vita wafungwe keshokutwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Umuhimu wa mchezo huo unatokana na ugumu wa Kundi D kwani kila timu iana nafasi ya kuendelea hatua ya robo fainali endapo itashinda mchezo wake wa mwisho.

Simba wanahitaji matokeo ya ushindi ili kufikisha pointi tisa ambazo zitawafanya waingie robo fainali huku wakisubiri mmoja kati ya Al Ahly na Saoura waungane naye.

AUSSEMS ALA KIAPO

Alisema wana kila sababu ya kuibuka na ushindi katika mchezo huo na wachezaji wake wana furaha na amani hali ambayo inamwaminisha kuibuka na ushindi katika mchezo huo.

“Tuna kila sababu ya kuibuka na ushindi katika mchezo huu kwa sababu ndio tiketi yetu ya kufuzu hatua ya robo fainali, ni jambo ambalo wote tunaamini tunaweza kulitekeleza,” alisema.

Akizungumzia wachezaji wake waliokuwa majeruhi pamoja na kukosekana kwa Jonas Mkude ambaye ana kadi tatu za njano, alisema marekebisho yote anayafanya kabla ya mchezo huo.

“Najua kuna wachezaji nitawakosa katika mchezo ujao lakini kesho (leo Jumatano) mazoezini nitajua naziba vipi mapengo hayo na kila kitu kitakaa sawa,” alisema.

Aussems aliongeza kwamba tatizo la kufungwa magoli ya krosi sio tatizo ambalo linatokea katika kikosi chake tu, ila anaendelea kupambana nalo ili kulimaliza kabisa

Nahodha wa Simba, John Bocco alisema wana morali kubwa ya kupata ushindi katika mchezo huo wa nyumba,

“Hatuna kitu tulichobakiza juu ya mchezo huu kwahiyo akili zetu na morali ya wachezaji wote ipo mchezo ujao.”

ISHU YA OKWI IPO HIVI

Mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi alitoa sintofahamu kwa wadau wa timu hiyo baada ya kukosekana kwenye kikosi kilichokwenda Algeria licha ya kuelezwa anaumwa na alikwenda kwao Uganda.

Mkurugenzi Mkuu wa Simba, Crescentius Magori aliliambia Mwanaspoti kuwa hajapata taarifa juu ya Okwi kwenda kwao na kuahidi kufuatilia ili kujua juu ya maendeleo ya afya yake.

“Kweli Okwi alikuwa hapatikani kwenye simu, lakini baadaye alikuja na alizungumza na kocha alimwambia anaumwa baada ya hapo tukamwacha, hizo taarifa za kwenda Uganda kisa kaitwa timu yake ya Taifa sifahamu lakini nitazifuatilia kwa ukaribu,” alisema.