Aubameyang auwasha moto wa Lacazette

Muktasari:

  • Takwimu hazidanganyi. Tangu Aubameyang atue Emirates akitokea Borussia Dortmund kwa dau la Pauni 56 milioni huku Lacazette (27) aliyesajiliwa kwa Pauni 46.5 milioni kutoka Lyon, mambo yamebadilika sana. Hata hivyo, ujio wa Aubameyang ambaye ni straika wa kimataifa wa Gabon, umemuweka Lacazette matawi ya juu na kuingia kwenye rekodi kibao barani Ulaya.

KAMA ulidhani kuondoka kwa Kocha, Arsene Wenger kuwa Arsenal ingeyumba kwenye kipute cha Ligi Kuu England, basi utakuwa umekosea sana kwani, ndio kwanza imewasha moto kinoma.

Lakini achana na mastaa wengine ambao wameifanya Arsenal kuwa moto kwelikweli, siri kubwa iko kwa wakali hawa Alexandre Lacazette na Pierre-Emerick Aubameyang.

Kwa sasa mastaa hawa wametengeneza kombinesheni matata katika safu ya ushambuliaji pale Emirates, ambayo imekuwa ikiwapa shughuli mabeki wa timu pinzani kwenye EPL.

Takwimu hazidanganyi. Tangu Aubameyang atue Emirates akitokea Borussia Dortmund kwa dau la Pauni 56 milioni huku Lacazette (27) aliyesajiliwa kwa Pauni 46.5 milioni kutoka Lyon, mambo yamebadilika sana. Hata hivyo, ujio wa Aubameyang ambaye ni straika wa kimataifa wa Gabon, umemuweka Lacazette matawi ya juu na kuingia kwenye rekodi kibao barani Ulaya.

Awali, Lacazette hakuwa na uhakika hata wa kuanza kwenye kikosi cha kwanza cha Wenger kutokana na kuanza kwa kuchechemea.

Lakini baada ya mabosi wa Arsenal kuvunja benki na kulipa Pauni milioni 56, zilitosha kabisa kumzindua Lacazette, kutoka usingizini, ukawa ni mwanzo wake wa kuzaliwa upya.

Hizi ni takwimu za Mfaransa huyo, kabla na baada ya ujio wa Aubameyang.

Kabla ya ujio wa Aubameyang

Maisha mapya ya Lacazette, Kaskazini mwa London, yalianza vizuri tu.

Akianza kwa kuifunga Leicester City. Wakati Aubameyang anatua, alikuwa na mabao tisa katika michezo 27 (dakika 1,919), sawa na bao moja ndani ya dakika 213.2.

Hata ule uamuzi wa kumpanga katika eneo la pembeni, mara nyingi alipoingia akitokea benchi, haukumsaidia sana zaidi ya kuchemsha tu.

Katika michezo hiyo 27, alisaidia kupatikana kwa mabao manne na hapo kuifanya rekodi yake kuwa ni bao au asisti moja tu ndani ya dakika 147.6.

Matokeo ya jumla yalionyesha katika michezo hiyo 27, Arsenal ilishinda mechi 13 ikiwa ni sawa na asilimia 48.1 ikifunga mabao 46 (wastani wa bao 1.7 kwa kila mechi) huku ikiruhusu wavu wake kutikiswa mara 38 ikiwa ni wastani wa bao 1.4 kwa mechi.

Baada ya ujio wa Aubameyang

Lakini mara baada ya Aubameyang kutua Emirates, kumeongeza ushindani wa namba katika ndani ya Arsenal huku ukiimarisha zaidi utendaji kazi wa Mfaransa huyo.

Ukiangalia kiwango chake msimu uliopita, baada ya ujio wa Aubameyang, kabla ya ujio wa Kocha, Unai Emery, utagundua kuwa tayari Lacazette alikuwa ameshaanza kushika kasi.

Kati ya Januari 31, Aubameyang alipotua Emirates hadi mwisho wa msimu, aliingia dimbani mara 11 (dakika 896).

Licha ya kuandamwa na majeraha ya kila mara, straika huyo alifunga mabao manane, akiweka wastani moja ndani ya dakika 112. Wastani wake wa kufunga bao ukiimarika maradufu ikiwa ni sawa na bao moja ndani ya dakika 100 tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

Hata hivyo, alitoa asisti moja tu. Msimu huu wa 2018-19 baada ya ujio wa Emery, ambaye ameibadilisha Arsenal na kuifanya kuwa moto na Lacazette amefunga mabao sita na asisti nne, katika michezo 14 (dakika 859).

Hii ni sawa na wastani wa bao moja ndani ya dakika 85.9. Kwa jumla takwimu zinaonyesha ujio wa Aubameyang ulimsukuma Lacazette kufunga walau bao au kutoa asisti moja ndani ya dakika 92.4, ikiwa ni rekodi bora ikilinganishwa na wastani wa bao au asisti moja, ndani ya dakika 147.6 ya awali.

Katika mechi alizocheza Lacazette, Arsenal imeandikisha rekodi ya wastani wa mabao 2.4, kwa kila mechi (ongezeko la wastani wa 0.7), wakifugwa bao 1.2 kwa kila mechi (idadi hiyo ikishuka kwa wastani wa 0.2) wastani wa kupata ushindi ukiongezeka hadi asilimia 68 kutoka 48.1.

Kwa moto ambao Arsenal imeuwasha kwa sasa, hata kelele za mashabiki wake zimeshika kasi wakitaka kukutana na klabu kubwa kama Manchester United, Chelsea au Man City kwani, wana uhakika wa kufanya kweli zaidi ya hapo.