Atapeli maduka baada ya kufanana na Pirlo

Muktasari:

Kwa kufanya hivyo, Palazzolo alikuwa akimdhalilisha Pirlo na familia yake. Pirlo ni mmoja kati ya mastaa wachache katika soka ambao wametokea katika familia tajiri. Baba yake alianzisha kampuni ya masuala ya chuma katika mji wa Brescia mwaka 1982 iliyoitwa Elg Steel.

TURIN, ITALIA.STAA wa zamani wa kimataifa wa Italia, Andrea Pirlo aliyetamba na klabu za Inter Milan, AC Milan na kisha Juventus anamshtaki mtu aliyefanana naye ambaye amekuwa akitumia mfanano huo kutapeli katika maeneo mbalimbali nchini Italia.

Mtu huyo ambaye anajifanya kuwa yeye ni Pirlo amekuwa akipokea nguo na vito mbalimbali kwa kipindi cha miaka miwili sasa huku akijifanya eti kuwa yeye ni Andrea Pirlo, staa wa soka aliyetamba nchini Italia.

Mtu huyo mwenye umri wa miaka 48 ametambulika kama Alessandro Palazzolo anayetokea mji wa Valenza nchini humo Italia amekamatwa na polisi wa Turin huku akishtakiwa kwa kosa la utapeli akitumia sura ya Pirlo.

Upelelezi wa kukamatwa kwake ulianza wakati Pirlo alipopeleka malalamiko yake ya kudaiwa vitu mbalimbali na maduka ambayo hakuwahi kuyakopa kitu chochote na ndipo Polisi nchini Italia walipoingia kazini kufanya uchunguzi.

Inadaiwa kwamba Palazzolo alikuwa akiwadanganya wenye maduka katika miji ya Turin, Brescia na Napoli, huku akiomba mapunguzo makubwa ya bei pamoja na upendeleo maalumu huku kuna wakati akichukua vitu bure kwa madai ya kulipa siku za usoni. Kote huko aliaminika kwa sababu alikuwa amefanana vilivyo na Pirlo.

Hata hivyo, Palazzolo hakuweza kurudisha vitu hivyo dukani na alishindwa kabisa kulipa ingawa bidhaa zenyewe zilikuwa ghali. Kama vile haitoshi, mtu huyu alijaribu kupata huduma za kitabibu bure kutoka kwa daktari wa zamani wa staa huyo.

Kitu kibaya zaidi ni pale ambapo Pirlo alijikuta akiingia matatani kwa wauza maduka hayo ambapo mara kadhaa walimfukuzia na kumtaka awalipe bidhaa ambazo alikuwa amekopa. Kitu hicho kilimkera kwa sababu hakuelewa kilichokuwa kinaendelea.

Baadaye Polisi walifanikiwa kumtia nguvuni Palazzolo baada ya kumnyatia katika mawasiliano yake ya simu kwa msaada mkubwa wa wauza maduka hayo na alipopatikana walithibitisha kwamba alikuwa ni yeye aliyewatapeli kutokana na kufanana kupitiliza na Pirlo.

Kwa kufanya hivyo, Palazzolo alikuwa akimdhalilisha Pirlo na familia yake. Pirlo ni mmoja kati ya mastaa wachache katika soka ambao wametokea katika familia tajiri. Baba yake alianzisha kampuni ya masuala ya chuma katika mji wa Brescia mwaka 1982 iliyoitwa Elg Steel.

Pirlo mwenyewe ana hisa katika kampuni hiyo na katika biashara za familia lakini pia amekusanya kiasi kikubwa cha pesa katika katika maisha yake ya soka ingawa katika mahojiano yake na jarida la Vanity Fair la nchini Italia aliwahi kukaririwa akidai kwamba hataki sana kuongelea masuala yanayohusu pesa.

Pirlo anajulikana kwa kupenda biashara ya mvinyo ambapo mpaka sasa anaendesha kiwanda chake cha mvinyo nchini Italia ambacho kinazalisha chupa 15,000 hadi 20,000 kwa mwaka.

Pirlo ambaye alistaafu soka mwaka 2017 akiwa na klabu ya New York City ya Marekani aliwahi kushutumiwa kwa kucheza na glasi ya mvinyo mkononi katika kipindi cha pili cha pambano dhidi ya Orlando City. Licha ya kupika mabao mawili akiwa na glasi mkononi lakini alishutumiwa na wapinzani wake kwa kuwadharau.

Katika familia Pirlo amezaliwa pamoja na kaka yake tu aitwaye Ivan.

Alioa mke wa kwanza Deborah Roversi mwaka 2001 na wana watoto wawili, Niccolo aliyezaliwa mwaka 2003 na Angela aliyezaliwa mwaka 2006.

Mwaka 2014 aliachana na Roversi baada ya miaka 13 ya ndoa yao kufuatia uhusiano wake na mrembo Valentiba Baldini aliyekutana naye wakati wanacheza gofu.