Arrizabalaga afanya kweli akiwa Hispania

Lisbon, Ureno. Kepa Arrizabalaga amefanikiwa kumaliza dakika 90 bila kuruhusu bao katika mchezo wa suluhu wa timu yake ya taifa ya Hispania dhidi ya Ureno juzi usiku.

Cristiano Ronaldo angeweza kumfunga kipa huyo aliyepoteza namba katyika kikosi cha cha Chelsea, lakini alikataliwa na mlingoti wa goli.

Kepa ameenguliwa kama kipa namba moja na kocha wa Blues, Frank Lampard kutokana na kufanya makosa mfululizo katika kikosi cha miamba hiyo ya London.

Kipa mpya, Edouard Mendy ameanza kujitengenezea jina katika nafasi ya kipa namba moja wa Chelsea baada ya kusajiliwa na miamba hiyo ya Kaskazini mwa London tangu aliposajiliwa kutoka Rennes.

Lakini kocha wa timu ya taifa ya Hispania, Luis Enrique alimwamini Kepa na kumwanzisha katika mchezo wa juzi badala ya David De Gea.

Ronaldo na washambuliaji wenzake wa Ureno walifanikiwa kupiga shuti moja pekee langoni, lakini hilo bado lilimwacha Kepa kutoruhusu bao katika mchezo huo.

Nyota huyo wa Juventus mwenye miaka 35, alikaribia kufunga bao la kuongoza kwa Ureno baada ya kugongesha nguzo mapema kipindi cha pili.

Baada ya kumiminwa krosi katika eneo la hatari, Ronaldo aliutuliza kabla ya kuachoa shuti lililogonga nguzo.