Antony Mavunde alimsha dude Yanga

Tuesday March 12 2019

 

By Matereka Jalilu

DODOMA. SIKU chache baada ya kuteuliwa kuongoza Kamati Maalumu ya Kuhamasisha Uchangishaji wa fedha Yanga, Anthony Mavunde ambaye ndiye mwenyekiti wa kamati hiyo ameahidi kuhakikisha lengo la uongozi wa timu hiyo linafanikiwa ikiwemo kuondokana na changamoto ya kiuchumi inayoikumba.

Mavunde ambaye ni Mbunge wa Dodoma Mjini na Naibu Waziri wa Kazi Ajira na Watu Wenye Ulemavu, anaiongoza kamati hiyo ya watu 26 na ameliambia Mwanaspoti amekubaliana na uteuzi huo na atahakikisha anafanya kila linalowezekana kufanikisha lengo la Yanga.

“Nimepokea kwa mikono miwili heshima hii, nitahakikisha lengo la kamati hii linafikiwa, nitapambana kwa kila hali nikishirikiana na wanakamati wenzangu ili kuisaidia timu,” alisema.

Aliwaasa wanachama na wapenzi wa Yanga kote nchini kuungana nao na kushiriki kuchangia timu hiyo ili iendelee kufanya vizuri zaidi msimu huu ikiwemo kuchukua taji la Ligi Kuu na Kombe la FA.

Aidha Mavunde ambaye ni Mlezi wa Tawi la Yanga Makao Makuu, Dodoma aliwapongeza wanachama na wapenzi wa Mkoa wa Dodoma kwa kuwa mstari wa mbele kuichangia timu hiyo ambapo mwenyekiti wa tawi hilo, Dominic Albinus ‘Baba Paroko’ alikubali kuchangia Sh 1 milioni kila mwezi.

“Tawi letu chini ya mlezi wetu, Mavunde mbali na kuhamasisha wapenzi wa Yanga kuwa wanachama lakini pia kwa pamoja tumekubaliana kuchangia kila mwezi Sh 1 milioni kwa timu yetu ili iendelee kufanya vema zaidi msimu huu kwa kubeba mataji na kufanya usajili wa msimu ujao,” alisisitiza.

Advertisement