Ambundo: Corona imechelewesha ubingwa wa Gor Mahia

Sunday April 05 2020
Gorpic

Dar es Salaam. Mshambuliaji wa Kimataifa wa Tanzania, Dickson Ambundo anayeichezea kwa mkopo Gor Mahia akitokea Alliance ya Mwanza, amesema kama sio janga la corona basi Aprili ulikuwa mwezi wa kujihakikishia kutetea ubingwa wao wa Ligi Kuu Kenya 'KPL'.

Gor Mahia wanaongoza msimamo wa Ligi Kuu Kenya wakiwa na pointi 54 ambazo wamezikusanya katika michezo 23, Kakamega Homeboyz wanawafuata wakiwa na pointi 47.

Ambundo alisema itabidi wasubiri hadi hali itakuwa shwari ili kujihakikishia ubingwa wa Ligi Kuu nchini humo kwa mara nyingine tena, utakuwa ubingwa wake wa kwanza akiwa na miamba hiyo.

"Kuchukua ubingwa ni shauku yangu lakini lazima tukubaliana na hiki ambacho kimetokea, hali si shwari, janga la corona limetibua kila kitu, kama si hivyo tungejiweka katika mazingira mazuri mwezi huu ya kuchukua ubingwa.

"Pamoja na kuwa huu ni msimu wangu wa kwanza itakuwa fahari kwangu na familia yangu kwa mafanikio ambayo nitakiwa nimeyapata," alisema nyota huyo wa Gor Mahia.

Kusimama kwa Ligi Kuu Kenya kumemfanya Ambundo kurejea nyumbani Tanzania ikiwa ni hatua ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona.

Advertisement

Pamoja na kuwa nchini kwa siku kadhaa sasa Ambundo alisema kuna program za mazoezi ambazo anaendelea nazo ili kujiweka tayari na patashika za Ligi Kuu Kenya zitakaporejea.

"Tutapewa taarifa za kuwa lini tutarejea Kenya. Maombi yangu ni kuwa hili janga lipite ili shughuli nyingine ziendelee," alisema.

Advertisement