Ambokile machungu ya Ronaldo yamsukuma Mazembe

Tuesday July 16 2019

 

By Eliya Solomon

KUNA kisa kimoja kinamhusu supastaa wa Juventus, Cristiano Ronaldo alipokuwa Manchester United yani kimempa mzuka wa kutosha Eliud Ambokile ambaye hivi karibuni alijiunga na miamba ya soka ya DR Congo, TP Mazembe.

Kupitia kituo cha luninga cha ITV nchini England, Patrick Evra ambaye alicheza na Ronaldo kuanzia 2006 hadi 2009, alisema Mreno huyo hakuna kitu kinachomnyima usingizi kama kushindwa.

Ilikuwa hivi, siku moja alicheza mchezo wa tenisi ya mezani na Rio Ferdinand walipokuwa United, kilichotokea kwenye mtanange huo alipoteza mchezo huo.

Jambo hilo lililonekana kumvuruga sana Cristiano. Alichoamua kufanya kwa siri ni kutafuta vifaa na kujifua kwa wiki mbili kunoa makali yake katika mchezo huo wa tenisi.

Baada ya kujiona yupo fiti, alipendekeza mpambano wa marudiano na Rio tena akitaka upigwe mbele ya umati wa watu. Na Matokeo yake…? Beki huyo wa zamani wa timu wa taifa ya England alikiona cha moto kutoka kwa Ronaldo.

Ambokile anasema siku zote amekuwa mjinga kila aendapo kwa kuanza kuwasoma wachezaji wenzake kujua madhaifu yao ili kujiweka tofauti nao kwenye vita ya kuwania namba kikosi cha kwanza.

Advertisement

Nyota huyo wa zamani wa Mbeya City, anasema tangu akiwa nyumbani Tanzania maisha yake yamekuwa kutokukubali kushindwa na tabia hiyo ilimsaidia kupata namba akitokea kikosi cha vijana na mwishowe kuwa mchezaji wa kutegemewa.

Mshambuliaji huyo mpya wa TP Mazembe ya DR Congo, anasema shuku yake ni kutaka kutengeneza utawala wake kwa mabingwa wa kihistoria nchini humo kama ilivyokuwa kwa Mbwana Samatta.

TP Mazembe ambayo waliichezea Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu ni mabingwa wa kihistoria nchini DR Congo kutokana na kutwaa kwao ubingwa wa Ligi Kuu ‘Linafoot’ mara 16.

Ambokile ambaye msimu uliopita aliifungia Mbeya City mabao 10 katika Ligi Kuu Tanzania Bara, amejiunga na TP Mazembe kwa kusaini mkataba wa miaka mitatu.

Nyota huyo anasema amepambania nafasi ya kutaka kucheza soka la kulipwa kwa kipindi kirefu hivyo anamshukuru Mungu kwa nafasi aliyoipata ya kujiunga na TP Mazembe.

“Samatta anaheshimika Mazembe, hakuna asiyejua habari zake, alifanya kwa nafasi yake na mimi nataka kufanya kwa namna yangu, wanavyomchukulia itabaki hivyo na mimi wataniona kwa tofauti.

“Sipendi kufananishwa na Samatta, lakini nahitaji kufuata hatua alizopita kwa sababu ni mfano mzuri kwetu ambao tunachipukia, nitajitahidi kujifunza kwa haraka ili niendane nao,” anasema mshambuliaji huyo.

Samatta akiwa na TP Mazembe ametwaa Ligi Kuu mara tano katika miaka ya 2011, 2012, 2013, 2014 na 2016, Kombe la FA nchini humo mara tatu, 2013, 2014 na 2016, Ligi ya Mabingwa 2015 na Kombe la Shirikisho Afrika 2016.

Mafanikio binafsi aliyoyapata akiwa na TP Mazembe ni kuwa Mchezaji Bora wa Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani 2015 na pia ndani ya mwaka huo Samatta alikuwa mfungaji bora wa Ligi ya Mabingwa Afrika na mwaka uliofuata alichagulia katika kikosi bora cha CAF.

Ambokile mwenye umri wa miaka 25 anasema malengo aliyojiwekea ni kucheza Ligi ya Congo kwa misimu miwili hadi mitatu na baada ya hapo atimkie zake barani Ulaya.

Mshambuliaji huyo, ameweka wazi sababu zilizomfanya ajiunge na TP Mazembe kuwa ni kutokana na mafanikio ambayo wamekuwa wakiyapata katika mashindano mbalimbali ya kimataifa ambayo anaona yanaweza kuwa daraja kwake la kupiga hatua.

“Kama watu wanakumbuka kile kipindi ambacho Samatta alikuwa akifanya vizuri pia TP Mazembe nao walikuwa katika kiwango cha juu, kufanya kwake vizuri kulimfanya aonekane na akaondoka kwa kwenda Ubelgiji.

“Naamini naweza kuwa na maisha mazuri, muda ukapofika naweza pia kuondoka na mimi, najua kama kuna kazi kubwa mbele yangu, lakini nitapambana, nilikuwa na nafasi ya kujiunga na Black Leopards ila nimeiona kupitia Mazembe nitaonekana zaidi,” anasema.

Akiwazungumzia wachezaji ambao tayari ameanza nao mazoezi katika maandalizi ya awali kuelekea msimu msimu mpya wa Ligi Kuu nchini humo, Ambokile anasema wamekuwa wakimpa ushirikiano wa kutosha.

“Kuna vitu ambavyo tunafanana, hapa nazungumzia tabia na tamaduni zetu, Watanzania na Wacongo tunapishana padogo sana, wachezaji wengi wamenichangamkia na wameniambia nijione kuwa nipo nyumbani.

“Asilimia kubwa wanaongea Kiswahili, nasubiri kukutana na mastaa wa timu ambao wenyewe wapo katika mapumziko, bado kambi rasmi haijaanza na ukizingatia kuna fainali za AFCON zinaendelea Misri,” anasema.

Ambokile atawania namba dhidi ya Meschack Elia, Mputu Tresor na Muleka Jackson kikosini.

Kabla ya kujiunga na TP Mazembe, Ambokile ambaye yupo chini ya kampuni ya usimamizi wa wachezaji ya Siyavuma, aliwahi kufanya majaribio ya siku tano kwaajili ya kujiunga na El Gouna FC inayoshiriki Ligi Kuu Misri.

Kwa sasa Ambokile yupo zake Rwanda na Mazembe ambako wanashiriki Kombe la Kagame, anadai kuyachukulia mashindano hayo kama sehemu ya kuzoeana na wenzake kabla ya kuuanza msimu ujao wa 2019/20.

Advertisement