Alliance Girls yapania kuisambaratisha Simba Queens

Muktasari:

Alliance Girls inakwenda katika mchezo huo ikiwa inaongoza ligi kwa pointi 25 wakifuatiwa na Simba wenye alama 23.

Mwanza. Kocha wa Alliance Girls, Ezekiel Chobanka amejitamba timu yake kuondoka na ushindi katika mchezo wa kesho dhidi ya Simba Queens katika Ligi Kuu ya wanawake.

Alliance Girls inakwenda katika mchezo huo ikiwa inaongoza ligi kwa pointi 25 wakifuatiwa na Simba wenye alama 23.

Chobanka alisema mchezo huo utakuwa mgumu kwao kwani wakipoteza basi Simba wataongoza ligi hivyo wanahitaji kupambana kuhakikisha wanapata ushindi.

Alisema kikosi chake kipo sawa tayari amewaambia nyota wake ugumu wa mchezo na jinsi gani pointi tatu zitakavyokuwa muhimu kwao.

"Timu iko sawa sina hata majeruhi mmoja na tayari tuko hapa Dar es Salaam kikubwa tumekuja kupata ushindi katika huu mchezo tunaomba mashabiki watupe sapoti" alisema Chobanka.

Alisema msimu huu wamejipanga kumaliza ligi hiyo wakiwa hawajapoteza hata mchezo mmoja na sasa wamebakiza mechi mbili kumaliza mzunguko wa kwanza.