Alliance Girls yafanya mauaji Ligi ya Wanawake

Tuesday July 7 2020

 

By James Mlaga

LICHA ya kuibuka na ushindi wa mabao 11-1 dhidi ya Panama Queens kwenye uwanja wa Nyamagana Jijini Mwanza jana, Kocha wa Alliance Girls Ezekiel Chobanka amesema kikosi chake kimecheza chini ya kiwango.

Ushindi huo ambao haujamfurahisha Chobanka, umeifanya Alliance Girls kufikisha pointi 31 na kuendelea kusalia katika nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu.

Akizungumza na Mwanaspoti, Chobanka amesema bado ana kazi kubwa ya kukinoa kikosi chake kwa kuwa Wachezaji wake wengi wameshuka kiwango na wengine wamekuwa wazito tofauti na ilivyokuwa mzunguko wa kwanza.

"Namshukuru Mungu tumepata alama tatu, lakini sijafurahishwa na aina ya uchezaji wa nyota wangu. Walikuwa wazito sana. Nimelazimika kufanya mabadiliko mengi ili kumpima kila Mchezaji" amesema Chobanka.

Ameongeza baada ya ushindi huo  sasa wamepata nguvu ya kuwania ubingwa wa mashindano hayo kwani mchezo uliopita walipoteza kwa jumla ya mabao 2-1 dhidi ya Kigoma Sisterz kwenye uwanja wa Lake Tanganyika Kigoma.

Mabao ya Alliance hii jana yamefungwa na Aisha Khamisi aliyepachika mabao sita, kiungo mshambuliaji, Aisha Juma aliyefumania nyavu mara nne na beki wa kulia, Sarah Joel aliefunga bao Moja.

Advertisement

Advertisement