Aliyemponza Mkude Stars afunguka

Saido Ntibazonkiza ni kiraka mpywa wa Yanga aliyesajiliwa siku moja baada ya kuitungua Taifa Stars bao 1-0 ameweka wazi kuwa Kocha Cedrick Kaze ndiye aliyemshawishi asaini Jangwani aje kumrahisishia kazi. Kaze anatua nchini kesho saa 4 usiku.

Huyu jamaa ndiye aliyemsababishia Kiungo wa Taifa Stars, Jonas Mkude kadi iliyopoteza ladha ya mchezo huo wa kirafiki na Watanzania tukalala pale kwa Mkapa.

“Unajua huu ni mpira nilijua kwamba ana kadi ya njano tayari na kuna muda nilimfanyia makosa, lakini naye akaonekana kutaka kulipiza. Ni mbinu za mchezo.

“Alipokuja kwangu hakuja vizuri na kama alionyesha hasira ndio maana mwamuzi aliweka ipigwe kwao.

“Nikaona bado ana moto nikazidi kumpa maneno ili mwamuzi amtulize kwa kadi, unajua hapo ni suala zima la uzoefu na kweli mwamuzi alishawishika akampa kadi ambayo ilikuwa ni njano ya pili na kuzaa nyekundu.

“Mwisho ikawa faida kwa timu yangu na tukapata nafasi ya kuwashambulia zaidi na kisha kupata bao.

Unajua ni muda tulikuwa hatujashinda tangu tutoke Fainali za Mataifa Afrika kule Misri,” aliongeza winga huyo, ambaye mbwembwe zake uwanjani kwenye dakika za lala salama ziliwakosha mashabiki.

Mchakato wa usajili wa Saido kutua Yanga ulifanyika kwa usiri mkubwa ambapo, hata baadhi ya vigogo ndani ya klabu hiyo wameshtukia baada ya kuona picha huku kazi imeisha mapema tu.