HISIA ZANGU: Aliyempeleka Yikpe Yanga pepo ataisikia tu

BADO naendelea kumtazama mshambuliaji wa Yanga anaiyeitwa Yikpe. Juzi kuna video yake ilikuwa inasambaa mitandaoni. Namna alivyokosa bao la wazi katika pambano kati ya Mwadui. Sijui alikuwa anafikiria nini? Au alikuwa anafikiria ‘kumuua’ golikipa?

Kuna watu wachache walisimama upande wake. kwamba hata wachezaji mahiri huwa wanakosa mabao ya wazi. Ndio ni kweli. Hata Lionel Messi na Cristiano Ronaldo huwa wanakosa mabao ya wazi. Hata hivyo utamlaumu vipi Lionel Messi akikosa bao la wazi wakati ana uhakika wa kukupatia mabao 40 kwa msimu?

Kwa Yikpe ni mwendelezo. Mwisho wa yote anaacha maswali mengi nyuma yake. Hivi Yikpe anakupa ubora gani uwanjani? Hakuna mchezaji aliyetimia. Kila mchezaji ana udhaifu wake uwanjani. Yikpe ni mmoja wao tu. lakini kila mchezaji ana uwezo wake fulani uwanjani.

Kwa mfano, kuna mshambuliaji ambaye ana kasi sana lakini katika eneo la lango hana maarifa. Wakati fulani tuliwaita hawa wachezaji jina la Kazibure. Kuna mshambuliaji ambaye anajua kufunga zaidi lakini nje ya eneo la lango hawezi hata kumpiga chenga mchezaji mmoja.

Kuna mchezaji ambaye hajui kufunga lakini anawapa shughuli mabeki. Yeye ndiye ambaye anatengeneza nafasi kwa wenzake kuweza kuokota mipira anayowania na kisha kufunga. Aina ya wachezaji pia wanakuwa wazuri hewani kiasi kwamba anaweza kudondosha kwa vichwa mipira mingi inayoelekezwa kwake.

Katika aina zote hizi za washambuliaji Yikpe hayupo. Labda tuulizane, ana ubora gani ambao wengine tumeshindwa kuuona. Kuna hii sifa ya kwanza. Kuna baadhi ya wachezaji waliwahi kutokea hapa nchini na wengine nje ya nchi. Wazuri kwa kufukuza mipira lakini akili ya mwisho ni zero.

Kuna aina ya mchezaji anayejua sana kufunga lakini nje ya boksi sio hodari sana. Ni kama ilivyokuwa kwa Ruud Van Nisterlooy kule kwa wazungu. Aliweza sana kufunga lakini nje ya boksi hakuweza kupiga chenga hata wachezaji wawili. Hapa Yikpe hayupo.

Kuna mchezaji ambaye anaweza sana kuhangaishana na mabeki kwa ajili ya kuwasaidia wenzake. Kwa mfano, Emile Heskey alikuwa anashutumiwa kwa kutofunga mabao mengi akiwa na Liverpool. baadaye ikagundulika kwamba alikuwa anafanya kazi kubwa kwa ajili ya Michael Owen. Pindi ambapo Owen angemkosa Heskey uwanjani basi alikuwa anapwaya.

Olivier Giroud pia ni mshambuliaji ambaye hafungi sana lakini ni bingwa wa kuiunganisha timu katika eneo la mwisho. Karibu kila mpira wa juu unaoelekezwa katika lango la adui yeye huusogeza kwa kichwa kidogo na kuwapelekea wenzake.

Giroud pia ni mzuri katika mipira ya chini. Anajua kuwaunganisha wenzake. Kocha wa timu ya taifa ya Ufaransa, Didier Deschamps ni shabiki mkubwa wa Giroud kwa sababu hiyo tu. Katika michuano ya Kombe la Dunia pale Russia, Giroud hakufunga bao lolote na Deschamps alisimama nyuma yake.

Deschamps pia amekuwa akikutana na lawama nyingi kwa kutowateua kikosini washambuliaji wanaofunga zaidi katika ligi zao kuliko Giroud lakini Mfaransa huyu wa Chelsea ameendelea kuwa chaguo la kwanza katika kikosi cha Deschamps.

Alexandre Lacazette wa Arsenal, Wissam Ben Yedder wa Monaco, pamoja na Karim Benzema mwenye kesi tofauti na hawa, wamekuwa wakifunga mabao mengi pengine kuliko Giroud lakini Descamps ameamua kumng’ang’ania Giroud zaidi kuliko hawa. Giroud huwa anampa kitu tofauti ambacho hawa wengine hawana.

Tujiuliza, Yikpe anaipa nini Yanga? Mabao? Hapana. Kuiunganisha timu eneo la mbele? Hapana. Kasi? Hapana. Anaipa nini? Hapa ndipo ninapomuwaza mtu ambaye alipiga dili la Yikpe kwenda Yanga. Pepo ataisikia tu. Amewatapeli Yanga.

Biashara mbovu ilianzia pale ambapo Yikpe mwenyewe aligoma kufanya majaribio. Nadhani alijijua. Hata hivyo, kwa mazingira ya nje tu yalikuwa yanaonyesha kwamba Yikpe ni tatizo. Mchezaji mwenye umbo kubwa na zuri kama lake, anayetoka katika taifa kubwa la kisoka kama Ivory Coast, mwenye umri wa miaka 25, anachezaji Tanzania badala ya kuwa Marseille ya Ufaransa au Stuttgart ya Ujerumani?

Mazingira ya nje tu yaliyonyesha kuwa mchezaji ni tatizo. Bado Yanga waliingia mkenge wa kumkubalia asifanye majaribio. Kinachoshangaza zaidi ni kwamba Yanga walikuwa wametoka kuachana na washambuliaji wao ambao waliamini kwamba walikuwa tatizo kwao mwanzoni mwa msimu huu. Kwanini walipoteza tena umakini kwa mara nyingi na kumchukua mchezaji ambaye hawakujithibitishia ubora wake? Unatoka kuruka mkojo unavamia kinyesi. Hili ni tatizo la klabu zetu. Hawana mfumo mzuri wa kusaka wachezaji wa kigeni.

Bahati mbaya kwa mabosi wetu wa hizi klabu ni kwamba pindi unapofanya makosa kuleta mchezaji mbovu wa kigeni huwa unagharamika zaidi kuliko ukikosea katika kumsajili mchezaji wa ndani.

Hawa wa ndani hauwalipii kibali. Hawa wa ndani hawazijui haki zao vema. Wengi huwa wanadhulumiwa. Kuanzia katika malipo ya kumchukua hadi katika kuvunja mkataba wake. Hawa akina Yikpe huwa wanakuja na Mawakala wasomi ambao wanajua sheria. Kuuvunja mkataba wa Yikpe sio kazi rahisi kama kuuvunja mkataba wa Adam Salamba.