Aliyedai kubakwa na Neymar matatani

Muktasari:

Kimwana huyo alifunguka katika mahojiano hii karibuni kuwa anakumbana na mitihani mikubwa tangu alipomtuhumu Neymar kumbaka mwanzoni mwa Juni.

RIO DE JANEIRO, BRAZIL.KIBAO kimepinduka. Polisi wa Brazil wanachunguza kama kimwana Najila Trindade Mendes de Souza alitoa tuhuma za uongo za kubakwa dhidi ya Neymar.
Supastaa huyo wa soka alikuwa akichunguzwa kwa tuhuma za kumbaka mwanamitindo huyo wa Brazil, lakini Jumatatu wiki hii, ilithibitishwa kwamba polisi wanaacha kuchukua hatua zaidi kuelekea kesi hiyo dhidi ya Neymar kutokana na kukosekana na ushahidi wa kutosheleza kumfungulia kesi staa huyo wa klabu ya PSG.

Binti huyo amekuwa akijichanganya katika maelezo yake kuhusiana na tukio hilo, jambo liliamsha shaka kama ni kweli alibakwa.
"Yeyote anayeleta uongo anaweza kuadhibiwa na ndiyo tunachunguza kuhusu hili," alisema Mkurugenzi wa Upelelezi.
Polisi pia walifungua mashitaka madogo dhidi ya mwanamitindo huyo Juni 12 baada ya kuwatuhumu kwa rushwa katika mahojiano na kituo cha televisheni.
"Polisi hununuliwa, sivyo?" kimwana huyo alijibu alipoulizwa kuhusu tuhuma za kuibwa kwa ‘tablet’ yake aliyodai ina ushahidi dhidi ya mchezaji huyo.
Kimwana huyo alifunguka katika mahojiano hii karibuni kuwa anakumbana na mitihani mikubwa tangu alipomtuhumu Neymar kumbaka mwanzoni mwa Juni.
Trindade alimtuhumu Neymar kumbaka katika hoteli ya mjini Paris Mei 15 alikoenda kwa mwaliko wa mwanasoka huyo.
Mrembi huyo mwenye umri wa miaka 26, anaamini amekuwa akinyimwa haki na vyo vya habari na mamlaka za usalama nchini Brazil.
"Naona kama wanatumia udhaifu wangu kunikandamiza," alisema.
"Inanisumbua kwa sababu watu bado hawataki kuamini lile jambo halisi lililotokea.
“Tangu tukio lile hakuna mtu aliyekuja kwangu na kunisaidia. Sipati sapoti yoyote kwa sababu ishu imemzunguka kipenzi chao Neymar.”