Ajibu mtamu kinoma, Yanga yaichakaza Alliance

Muktasari:

Yanga imeendeleza rekodi yake ya kutokufungwa katika Ligi Kuu msimu huu na sasa ipo nafasi ya pili katika msimamo wa ligi

Dar es Salaam.Mshambuliaji Ibrahimu Ajibu ameiongoza Yanga kuichakaza Alliance FC kwa mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Yanga ilipata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya vibonde na wageni wa Ligi Kuu Bara, vijana wa Alliance na kuzidi kuifukuzia Azam FC iliyopo kileleni na alama 21 baada ya usiku wa juzi kushinda mabao 2-1 dhidi ya African Lyon.

Ibrahim Ajibu 'Kadabra' aliendelea kuonyesha msimu huu alivyo moto baada ya kuasisti mabao mawili na kufunga moja na kufiklisha bao lake la tatu msimu huu huku akihusika na mabao 11 ya Yanga kati ya 14 yaliyofungwa mpaka sasa akiasisti mabao nane.

Ajibu alianza kwa kumpigia pasi ndefu Heritier Makabo aliyefunga kwa kichwa bao la kwanza dakika ya 17 likiwa la tatu kwake msimu huu, kabla ya kumpigia pasi ndefu Mrisho Ngassa aliyefunga la pili dakika ya 24. Bao hilo la kubetua lilikuwa la pili kwa Ngassa aliyerejeshwa Jangwani msimu huu akitokea Ndanda FC.

Dakika ya 86, Ajibu akamalizia udhia kwa kufunga bao la tatu kwa Yanga baada ya mabeki wa Alliance kuzembe kuokoa mpira langoni mwao na kuifanya Vijana wa Mwinyi Zahera kufikisha alama 19, mbili pungufu na ilizonazo vinara Azam.

Katika mechi nyingine zilizochezwa leo, Prisons ikiwa nyumbani ilibanwa na Singida United kwa kulazimishwa sare 0-0 matokeo ambayo yanafanana na yale ya Coastal Union 0-0 JKT Tanzania na Biashara 0-0 KMC.