Ajibu, Makambo waitikisa Yanga

Muktasari:

Katika kuhakikisha Yanga mpya inakuwa moto viongozi wa klabu hiyo wamepanga kukutana na Kocha Mwinyi Zahera ili kuwapa bajeti yake ya usajili.

MABOSI wapya wa Yanga wametikiswa. Unajua nini? Nyota wa timu hiyo wameichungulia ratiba ya Ligi Kuu na kubaini wamesaliwa na mechi mbili tu kabla ya kumaliza msimu, huku wakiwa wanaidai klabu hiyo malimbikizo mengi ya fedha.

Fasta nyota hao wakiwamo Ibrahim Ajibu, Heritier Makambo na wengine wanaona wafanye jambo moja ambalo litawashtua mabosi wao ili wamalizie chao mapema kwani wanaamini msimu ukiisha wanaweza kula za uso kupata fedha wanazodai.

Ndipo, wakapanga wafanye mgomo mwingine wa maana kwa mechi zao zilizosalia dhidi ya Mbeya City na Azam na ndipo taarifa hizo zikawafikia mabosi hao na kuitisha kikao cha dharura klabuni hapo ili kuweka mambo sawa hasa baada ya kuona chama lao bado lina nafasi ya kubeba ndoo kama watetezi wa Ligi Kuu, Simba watayumba kwenye mechi zao.

Chanzo kutoka ndani ya Yanga, kilivujisha siri kwa Mwanaspoti, nyota wa timu hiyo walikuwa wamepanga kufanya mgomo ili kushinikiza kulipwa bonasi za mechi zao nne zilizopita walizopigwa kalenda mbali na fedha za mishahara na zile za usajili.

Bonasi ambazo akina Makambo wanazililia ni zile za mechi zao dhidi ya Coastal Union, Ndanda, Prisons na Singida United.

Chanzo hicho kilisema baada ya viongozi wa Yanga kupata taarifa za mgomo huo waliwaita mastaa wao ili kuzungumza nao na kujua namna ya kuwapoza chochote. “Unajua wachezaji wanadai pesa zao kwa muda mrefu, ukweli wamekuwa wavumilivu wa hali ya juu kuendana na hali halisi ya klabu, ikumbukwe wanarejea majumbani kwao ambako wana majukumu dhidi ya familia zao, angalau wapewe chochote.

“Tulikubaliana ili wasicheze mechi mbili zilizobakia, kitu ambacho ni kigumu kwa klabu yetu ndio maana wamekuja (jana) ili kukutana na viongozi kwa ajili ya mazungumzo kujua kama kitapatikana chochote wapewe wakamalizie mechi hizo,” alisema.

Mmoja ya wachezaji wa timu hiyo (jina tunalo) alilidokeza Mwanaspoti baada ya kikao hicho kilichotumia saa moja, mabosi wao wamekubali kuwalipa fedha hizo za bonasi na kwa mechi walizoshinda kila mchezaji atapewa Sh100,000 na zile walizotoka sare wataambulia Sh50,000 na wote wamekubali kwa vile lengo ni kuona Yanga inamaliza ligi vizuri. “Kila kitu kimeenda sawa, viongozi wamekubali kutupa chetu, ila kwa ishu za mishahara na fedha nyingine wametuahidi kutumalizia taratibu nasi hatuoni sababu ya kuendelea na msimamo wa awali,” alilihakikisha Mwanaspoti.

ZAHERA BADO YEYE TU

Katika kuhakikisha Yanga mpya inakuwa moto viongozi wa klabu hiyo wamepanga kukutana na Kocha Mwinyi Zahera ili kuwapa bajeti yake ya usajili.

Awali Zahera alishatangaza ana majina ya wachezaji anaowataka na viongozi walisisitiza wapo tayarui kumsajili yeyote anayehitajiwa na kocha wao, lakini jana Mwenyekiti Dk Mshindo Msolla alisema ni lazima kwanza waijue bajeti nzima ilivyo.

“Mtu pekee mwenye jukumu la kufahamu ni kiasi gani kinatakiwa kutengwa kwa ajili ya usajili ni kocha, hivyo tumepanga kukaa na kocha mara baada ya mchezo wetu na Mbeya City ili aweze kupendekeza bajeti ambayo itaweza kusajili kikosi chenye ushindani.”

“Kuhusu kuwa na kamati ya usajili hili pia lipo katika mchakato kwani tayari tumeshateua baadhi ya wanayanga na tunaendelea na mazungumzo nao ili waweze kubeba jukumu la kamati hiyo ambayo ni muhimu sana na tuna imani nao kutokana na kuwa na vigezo vinavyotakiwa,” alisema. Pia aliongeza wanatarajia kutumia wachezaji wa zamani kuzunguka mikoani kuangalia vipaji vya wachezaji ambao wanaweza wakasajiliwa kuanzia vijana hadi kikosi cha kwanza na kuweka wazi Zahera mwenyewe hataweza.

KIHAMIA ARUDISHWA KUNDINI

Wakati huohuo Dk. Msolla amemteua Athuman Kihamia na Shija Richard kuwa wajumbe wa Kamati ya Utendaji wa Yanga wakifikisha idadi ya wajumbe kumi na kuweka wazi uteuzi wa nafasi hizo utaendelea baadaye.

“Kihamia sio mgeni katika kamati hiyo atatumia uzoefu wake kuwapa maelezo wajumbe ambao ni mara yao ya kwanza kuongoza kamati hiyo ambayo itapangiwa majukumu yao ya kufanya kadri muda unavyozidi kwenda,” alisema.