Aguero ni sumu Big Six England

Muktasari:

Aguero pia amekuwa kiboko ya Liverpool wanapokwenda kucheza kwenye Uwanja wa Etihad. Fowadi huyo amefunga katika mechi zote saba alizoichezea Man City dhidi ya Liverpool kwenye mechi ya Ligi Kuu England uwanjani Etihad.

MANCHESTER, ENGLAND.SUPA Sergio. Wanamwita hivyo, ukiweka kando ile a.k.a yake ya utotoni Sergio ‘Kun’ Aguero. Kwa kifupi tu ni bonge la straika linalobamba huko kwenye mikikimikiki ya Ligi Kuu England akitupia jezi za wababe wa Etihad, Manchester City.

Alhamisi iliyopita uwanjani Etihad, Aguero alipiga bonge la bao wakati kikosi chake cha Man City kilipoichapa Liverpool 2-1 na kuzirudisha mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu England kuwa tena na upinzani mkali.

Bao lake alilofunga kwenye mechi hiyo limemfanya Aguero kuwa mshambuliaji aliyefunga mabao mengi zaidi kwenye mechi za Big Six tangu kuanzia msimu wa 2011-12. Tangu wakati huo, Aguero amefunga mabao 37.

Mastaa wanaomfuatia kwa kufunga mabao mengi kwenye mechi zilizohusisha timu za Big Six tangu msimu wa 2011-12 ni straika Harry Kane, amefunga mabao 21, Wayne Rooney amefunga mabao 20, Robin van Persie amefunga mabao 18 na supastaa wa Chelsea, Eden Hazard amefunga mabao 17.

Aguero pia amekuwa kiboko ya Liverpool wanapokwenda kucheza kwenye Uwanja wa Etihad. Fowadi huyo amefunga katika mechi zote saba alizoichezea Man City dhidi ya Liverpool kwenye mechi ya Ligi Kuu England uwanjani Etihad.

Bao lake la Alhamisi iliyopita limemfanya awe amefikisha mabao 250 aliyofunga kwenye mechi za ligi. Aguero amefunga mabao 153 kwenye ligi akiwa na kikosi cha Man City, lakini alipokuwa Atletico Madrid alifunga mabao 74 kwenye La Liga na Independiente alifunga mabao 23 kwenye Ligi Kuu Argentina.

Rekodi zake za mabao kwenye kikosi cha Man City, kwa mguu wa kushoto amefunga mabao 28 na mguu wa kulia amefunga mara 110.

Aguero pia ni matata kwa mipira ya juu, ambapo amefunga kwa kichwa mabao 15, huku ndani ya boksi akifunga mara 135 na nje ya boksi amefunga mabao 18. Kwenye rekodi zake katika kikosi cha Man City, timu ambayo Aguero ameitesa sana kwa kuifunga ni Newcastle United, aliyoifunga mabao 14.