Afcon 2019: Taifa Stars ndani ya Cairo baada ya miaka 39

Monday April 15 2019

 

Dar es Salaam. Shirikisho la Soka Afrika (CAF) Ijumaa iliyopita lilitangaza droo kwa mataifa 24 yaliyofuzu kwa Fainali za Afrika 2019 zitakazoanza Juni 21 kule Cairo, Misri.

Mechi zimepangwa kufanyika kwenye Viwanja vya Cairo, Air Defense, Al Salam, Alexandria, Suez na Ismailia. Uwanja wa Cairo utachezwa mechi mbili, ufunguzi na fainali.

Kundi A kuna timu za: Misri, DR Congo, Uganda, Zimbabwe ambazo mechi zake zitachezwa kwenye Uwanja wa Cairo.

Kundi B lenye timu za: Nigeria, Guinea, Madagascar na Burundi zitakuwa Alexandria wakati Kundi C linaloundwa na: Senegal, Algeria, Kenya na Tanzania zitakuwa kwenye Uwanja wa Jeshi la Anga unaoitwa, Air Defense Stadium

Mechi za Kundi D zitaundwa na: Morocco, Ivory Coast, Afrika Kusini na Namibia zitakazochezwa Uwanja wa Al Salam wakati Kundi E linaundwa na Tunisia, Mali, Mauritania na Angola zitakuwa Uwanja wa Suez.

Kundi F lenye: Cameroon, Ghana, Benin na Guinea-Bissau mechi zake zitafanyika Uwanja wa Ismailia.

Misri ilishinda nafasi ya uwenyeji baada ya kuibwaga Afrika Kusini na ni kutokana na Cameroon iliyokuwa mwenyeji kuchemka katika maandalizi.

Pamoja na Misri kuwa mwenyejji wa fainali za mwaka huu, imekuwa na mafanikio katika michuano hiyo, imetwaa ushindi mara saba ikiwemo kutwaa mara tatu mfululizo kati ya 2006 na 2010.

Tangu mwaka 1996, mataifa 16 yalikuwa yakishiriki fainali hizo, lakini kwa mara ya kwanza mwaka huu, mataifa 24 yatapambana kwenye fainali za mwaka huu 2019.

UWANJA

Timu za Kundi C ikiwemo Tanzania zitakuwa kwenye Uwanja wa 30 ambao uko katikati ya jiji la Cairo. Uwanja huu unamilikiwa na Jeshi la Anga la Misri.

Umezoeleka kuitwa Uwanja wa Air Defense Sport Village.

MIAMBA YA KUNDI C

Algeria ‘Desert Foxes’

Moja ya timu za Kundi C zinazopewa nafasi ya kutikisa katika fainali za mwaka huu.

Ni wazoefu wa fainali za Afrika lakini pia iliwahi kukata tiketi ya Kombe la Dunia mwaka 1982, 1986, 2010 na 2014.

Algeria ilitwaa ubingwa wa Afrika mwaka 1990, walipokuwa wenyeji. Wakati wa

Fainali za Kombe la Dunia 2014, Algeria ilikuwa timu ya kwanza kufunga mabao manne dhidi ya Korea Kusini.

Algeria inafahamika kwa kuiharibia Ujerumani Magharibi mwaka 1982 kwa kuilaza mabao 2-1 kwenye kundi lao pamoja na Austria na Chile lakini pamoja na hayo timu hiyo ilitolewa.

Fainali za Afrika 1990

Algeria ilikuwa mwenyeji wa fainali za Afrika 1990 na ilipewa nafasi ya kutwaa ubingwa. Ilipangwa Kundi A, ikianza kwa kuilaza Nigeria 5–1, Ivory Coast 3–0, na ikailaza Misri 2–0. Ilitwaa ubingwa mwaka huo uliokuwa wa mafanikio.

Mwaka 1992 ilishindwa kujitetea na kutolewa raundi ya kwanza kama ilivyokuwa pia fainali za 1994 Algeria kutokana na kuchezesha ‘mamluki’ kwenye mechi za awali.

Mwaka 1996, Algeria iliingia tena  lakini ikatolewa na Afrika Kusini robo fainali. Ilishindwa kufuzu fainali za 1998, 2002 na 2006.

Tangu kipindi hicho haikufanya viuri japokuwa ilikuwa ikiingia fainali. Mwaka 2017 na 2018 kocha mpya, Christian Gourcuff alipingwa vikali baada ya Algeria kufungwa 2–1 na Guinea na sare ya 2–2 na Tanzania. Hata hivyo, ilipoilaza 7–0

Tanzania ikakata tiketi ya kucheza Kombe la Dunia 2018.

Wachezaji 26 wametajwa kwa ajili ya timu hiyo kujiandaa na Afcon na kati ya hao ni wachezaji watano tu wanacheza nje ikiwemo ligi zote tano kubwa duniani.

Senegal ‘Simba wa Teranga’

Walianza kucheza fainali za Afrika kwa mara ya kwanza mwaka 1965, wakimaliza wa nne baada ya kufungwa bao 1–0 na Ivory Coast.

Mwaka huu Ivory Coast iko Misri ikiwania ubingwa ikipangwa na Tanzania, Kenya na Algeria.

Fainali za 1990 Senegal ilimaliza ya nne na ilikuwa mwenyeji Fainali za 1992 lakini ilitolewa na Cameroon robo fainali. Senegal imefuzu mara nne kati ya fainali za Afrika ndani ya miaka 10.

Rekodi Bora

Senegal ilimaliza vizuri mwaka 2002, lakini ilipoteza kwenye fainali mbele ya Cameroon baada ya suluhu ya dakika 90. Mwaka huo pia ilifika robo fainali ya Kombe la Dunia ikizifunga Ufaransa, Denmark na Uruguay, na baadaye Sweden na kufungwa na Uturuki robo fainali

Fainali za 2008 ilimaliza ya tatu na ilishindwa pia kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia 2010. Mwaka huo, Senegal ilitolewa mapema Fainali za 2012 haikufanya vizuri.

Miamba hiyo ilizikosa fainali za Kombe la Dunia 2014 baada ya kupoteza kwa Ivory Coast raundi ya mwisho. Senegal ilifuzu mara mbili tangu mwaka 2015 lakini ikafanya vizuri mwaka 2017.

Novemba 10, 2017, Afrika Kusini ililala 2–0 na Senegal kufuzu Kombe la Dunia  2018, ikiwa ni mara ya pili tangu Fainali za 2002 Korea Kusini na Japan.

Senegal iliilaza Poland 2–1 moja wakijifunga na lingine la M’Baye Niang.

Senegal ilitoka sare ya 2–2 na Japan kwa mabao ya Sadio Mané na Moussa Wagué.Ilipigwa bao 1-0 na Colombia na hata hivyo miliaga hatua ya makundi.

Kenya, Harambee Stars

Ni timu kutoka Ukanda wa Cecafa. Kenya haina historia ndefu katika fainali za Afrika  ikiingia mara tano japokiwa imekuwa ikiishia hatua za awali.

Timu hiyo ambayo kwa sasa wananolewa na Mfaransa, Sébastien Migné ameiwezesha timu hiyo kufuzu baada ya kuzifunga Ethiopia na Ghana nyumbani na kutolewa kwa Sierra Leone kuliibeba timu hiyo na kufuzu fainali mapema.

Taifa Stars itaanza harakati zake za katika mashindano ya Afcon 2019 kwa kuwavaa Senegal katika mchezo wa ufunguzi wa Kundi C Juni 23 kwenye Uwanja wa Cairo.

Baada ya mchezo huo vijana wa Emmanuel Amunike watarudi uwanjani Juni 27 kuwavaa majirani zao Kenya katika mchezo unaotegemewa kuwa na upinzani mkali kila timu ikitaka ushindi ili kujiweka vizuri katika kundi hilo.

Tanzania itacheza mechi yake ya mwisho ya Kundi C kwa kuwavaa Algeria Julai Mosi katika mchezo unaotegemewa kuwa na ushindani wa aina yake kutokana na rekodi ya timu hizo kila zinapokutana.

Ratiba ya Kundi C

Juni 23: Senegal - Tanzania

Juni 23: Algeria - Kenya

Juni 27: Senegal - Algeria

Juni 27: Kenya - Tanzania

Julai 1: Kenya - Senegal

Advertisement