Afcon, Chan zasogezwa mbele

Tuesday June 30 2020
cHAN PIC

Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf) leo limefikia uamuzi wa kusogeza mbele mashindano yake mawili huku likifuta mengine kutokana na athari za mlipuko wa virusi vya Corona.
Taarifa kutoka katika kikao cha kamati ya utendaji ya Caf kinachoendelea kwa njia ya mtandao, zimefichua kuwa mashindano ya Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (Chan) yaliyokuwa yafanyike Aprili mwaka huu yamesogezwa mbele hadi Januari 2021.
Mashindano hayo ambayo yamepangwa kufanyika huko Cameroon kuanzia kati ya Januari hadi Februari mwakani
Mbali na Chan, kikao hicho cha kamati ya utendaji ya Caf pia kimeamua kusogeza mbele fainali za mataifa ya Afrika (Afcon) kutoka mwaka 2021 uliopangwa zifanyike hadi 2022 ambapo zitachezwa kati ya Januari na Februari.
Kamati hiyo ya utendaji ya Caf, imeamua pia kufuta mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (Awcon) yaliyokuwa yafanyike mwaka huu.
Kwa upande wa mashindano ya ngazi ya klabu, Caf imeamua mechi za hatua ya nusu fainali na fainali zote zitafanyika nchini Cameroon na zitachezwa kwa mkondo mmoja badala ya mechi mbili za nyumbani na ugenini kama ilivyokuwa hapo awali.
Uamuzi kama huo wa Ligi ya Mabingwa Afrika, umechukuliwa pia katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika ambalo litakuwa na mechi mojamoja tu za hatua ya nusu fainali na fainali ambazo zote zitachezwa nchini Morocco.

Advertisement