Afadhali Wanyama hakwenda Club Brugge

Muktasari:

Wanyama anaweza kucheza Leicester City, Everton, Wolves, West Ham na wengineo na tukaendelea kumuona kila mwisho wa wiki akicheza katika ligi ya kishindani. Msimu uliopita Victor alikaa nje kwa muda mrefu kutokana na kuwa majeruhi lakini aliporudi akaonyesha cheche zake.

SIJAWAHI kuelewa kwanini rafiki yangu, Victor Wanyama alitakiwa na Klabu ya Brugge ya Ubelgiji. Sijawahi kuelewa pia kwanini uhamisho haukutokea. Vyovyote vile, afadhali haukutokea. Wanyama saizi yake sio Brugge.

Unawezaje kutoka Tottenham kwenda Brugge? Unaweza kutoka timu ya Top Four England ukaenda timu iliyoshika nafasi ya pili Ubelgiji wakati ukiwa na miaka 28 kama pasipoti ya Victor Wanyama inavyosomeka? Inashangaza kidogo.

Afrika Mashariki inahitaji wachezaji wengi katika ligi kubwa za Ulaya, hasa Ligi Kuu ya England kwa ajili ya kuimarisha timu za taifa za ukanda huu. Ligi Kuu ya England ina timu nyingi achilia mbali zile zilizomo katika sita bora.

Wanyama anaweza kucheza Leicester City, Everton, Wolves, West Ham na wengineo na tukaendelea kumuona kila mwisho wa wiki akicheza katika ligi ya kishindani. Msimu uliopita Victor alikaa nje kwa muda mrefu kutokana na kuwa majeruhi lakini aliporudi akaonyesha cheche zake.

Inawezekana kwa sasa Kocha Mauricio Pochettino akawatumia zaidi Tanguy Ndombele na Giovani Lo Celso lakini safari ya kumaliza msimu ni ndefu. Tayari Lo Celso ameshaumia katika majukumu ya kimataifa. Hii ina maana kuwa nafasi ya Victor inazidi kusogea.

Lakini pia kuna michuano mbalimbali ipo njiani. Kombe la Ligi, FA na Ligi ya Mabingwa wa Ulaya. Lolote linaweza kutokea na Wanyama akapata nafasi yake na kurudi katika kikosi cha kwanza. Ni afadhali acheze bahati nasibu hii kuliko kurudi Ubelgiji.

Ubelgiji Wanyama alishawahi kucheza katika ardhi ya pale akiwa na Klabu ya Beerschot. Akaenda Celtic, akaenda Southampton na sasa yupo timu ya Top Four. Iweje ndani ya muda mfupi arudi tena Ubelgiji bila ya kufuata utaratibu maalumu wa kushuka.

Walau anaweza kuanza kushuka kwa kucheza Everton, kisha Celtic kabla ya kurudi Ubelgiji. Kama ofa ya Brugge ilikuwa nzuri kipesa na Wanyama anajiona hana cha kupoteza sana kucheza England basi ni afadhali angeenda China au Japan akalipwa zaidi tukajua kuwa ameondoka England kwenda ligi ndogo kwa sababu ya pesa. Swahiba wake, Moussa Dembele aliamua kufanya hivi mapema tu.

Afadhali Wanyama hakwenda Brugge. Sio timu ya saizi yake. Wakati watu wa Afrika Mashariki na kati tukifikiria mchezaji kama Mbwana Samatta aondoke Ubelgiji kwenda England, inakuwaje Wanyama arudi Ubelgiji?