Adama Traore awekwa mtegoni

 LONDON,ENGLAND. WINGA mwili jumba wa Wolves, Adama Traore atalazimika kufanya uamuzi mkubwa sana kwenye maisha yake ya soka baada ya kuitwa na timu za nchi mbili tofauti, Hispania na Mali ili kwenda kuzichezea kwenye soka la kimataifa.

Nchi hizo mbili zipo kwenye vita kali ya kusaka kibali cha mchezaji huyo kutumika kwenye mechi za kimataifa zitakazopigwa mwezi ujao.

Mali wanamtaka winga huyo mwenye kasi kubwa uwanjani kwenda kuchezea timu yao kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya Ghana, Oktoba 9 na dhidi ya Iran siku nne baadaye.

Hata hivyo, kocha wa Hispania, Luis Enrique naye amemjumuisha Traore kwenye kikosi chake cha awali kinachojiandaa na mechi ya kirafiki dhidi ya Ureno na mechi mbili za Nations League dhidi ya Uswisi na Ukraine.

Traore, 24, alizaliwa Hispania, lakini wazazi wake wote wawili wanatokea Mali.

Traore aliwahi kuitwa kwenye kikosi cha wakubwa cha Hispania, Novemba mwaka jana - lakini alijiondoa kwenye timu baada ya kuwa majeruhi.

Aliitwa tena na kocha Enrique mwezi Agosti, lakini alipofanyiwa vipimo na kukutwa na corona kabla ya mechi ilimlazimu kujiondoa kwenye timu.

Traore, ambaye alizitumikia timu za vijana za Hispania, atalazimika kutoa uamuzi wake wa mwisho wa nchi gani anataka kwenda kuiwakilisha kwenye soka la kimataifa. “Nimefurahi sana kuwa na nafasi ya kuchezea timu mbili,” alisema.