Werner, Cavani mpo? Mastraika hawa wametupia kwa fujo msimu wa kwanza Ligi Kuu England

LONDON, ENGLAND. DIRISHA la usajili la majira ya kiangazi limefungwa na sasa timu zote zinasubiri hadi Januari zitakapoingia sokoni kunasa mastaa wapya.

Kwa wachezaji ambao wamejiunga na timu mpya kwa sasa watakuwa na wajibu mkubwa wa kuhakikisha wanafanya vizuri ndani ya viwanja kusaidia timu zao.

Shughuli pevu kabisa inawakabili washambuliaji ambao watakuwa na wajibu wa kufunga mabao kusaidia timu. Kasheshe hilo linawakabili mastraika kama Timo Werner na Edinson Cavani, ambao huu ni msimu wao wa kwanza kwenye mikikimikiki ya Ligi Kuu England.

Kwenye kipute hicho kuna mastraika matata ambao wameonyesha ubora mkubwa kwenye misimu yao ya kwanza katika Ligi Kuu England wakiwa na timu mpya. Cavani na Werner wataweza kupita kwenye nyayo za mastraika hawa?

10) Yakubu - Portsmouth (mabao 16, asisti 1)

Mpeni mipira Yakubu, yeye atafunga tu. Hicho ndicho kilichokuwa kikisemwa wakati huo wakati Yakubu alipokuwa kikipiga Portsmouth. Straika huyo wa zamani wa Nigeria alitua Fratton Park kipindi hicho ikiwa inanolewa na Harry Redknapp na huko alionyesha kiwango bora kabisa wakati alipofunga mabao 16 na kuasisti mara moja kwenye msimu wake wa kwanza wa Ligi Kuu England. Staa huyo ni moja ya wachezaji waliotisha kwa kufunga kwenye misimu yao ya kwanza na timu mpya kwenye Ligi Kuu England, wakati huo alipokuwa akiitumikia Pompey.

9) Benni McCarthy - Blackburn (mabao 18, asisti 1)

Hakuwa mgeni kwa mashabiki wa soka wa England baada ya kufunga mara mbili dhidi ya Manchester United kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya kipindi hicho akiichezea FC Porto chini ya kocha Jose Mourinho katika mchezo uliopigwa Old Trafford mwaka 2004. Miaka miwili baadaye, Benni McCarthy alitua England kujiunga na Blackburn Rovers na kwenda kuendeleza yale makali yake ya kutupia baada ya kutua kwenye Ligi Kuu England. Msimu wake wa kwanza tu kwenye ligi hiyo, straika huyo wa zamani wa kimataifa wa Afrika Kusini alifunga mabao 18 na kuasisti mara moja, huku akiwa amezidiwa na Didier Drogba pekee yake kwenye mbio za Kiatu cha Dhahabu cha England.

8) Michu - Swansea (mabao 18, asisti 3)

Kwenye Ligi Kuu England aliwahi kutoka mkali matata kabisa, Michu, aliyekuwa akikipiga katika kikosi cha Swansea City, ambayo ilimsajili kutoka Rayo Vallecano mwaka 2012 kwenda kuchukua mikoba ya Gylfi Sigurdsson. Hakika usajili huo ulikuwa ulikuwa moto kabisa kwenye Ligi Kuu England, ambapo Michu kwenye mechi yake ya kwanza tu aliwasambaratisha QPR wakati alipofunga mara mbili kwenye ushindi wa 5-0 na baada ya hapo aliendelea kutupia na kumaliza msimu huo wa kwanza kwake kwenye ligi akiwa amefunga mabao 18 na kuasisti mara tatu.

7) Diego Costa - Chelsea (mabao 20, asisti 3)

Straika, Diego Costa alitua Chelsea akitokea kwa mabingwa wa Hispania kwa wakati huo, Atletico Madrid mwaka 2014 na hakika huduma yake baada ya kutua Stamford Bridge. Msimu wake wa kwanza kwenye Ligi Kuu England ulikuwa moto kabisa, ambapo alifunga mabao 20 na kuasisti mara tatu kipindi hicho alipokuwa akicheza chini ya Jose Mourinho. Mashabiki wa The Blues waliamini kwamba wamepata huduma bora kama ilivyokuwa kwa straika Didier Drogba na alionyesha ubora mkubwa baada kufunga mabao sbaa kabla hata ya kufika katikati ya Septemba na kuweka rekodi ya kufunga mabao mengi baada ya mechi nne.

6) Ruud van Nistelrooy - Man United (mabao 23, asisti 1)

Ni straika pekee aliyeonekana kama vile angemsumbua Thierry Henry mwanzoni mwa miaka ya 2000. Ruud van Nistelrooy alikuwa na umuhimu mkubwa sana kwenye kikosi cha Manchester United na hakika huduma yake ilikuwa moto mkali uwanjani. Straika huyo wa Kidachi, alitua Ligi Kuu England akiwa kwenye kasi ya hali ya juu, wakati alipofunga mara 23 na kuasisti mara moja katika msimu wake wa kwanza wa ligi akiwa na kikosi cha Man United. Ujio wake huko Old Trafford uliwafanya mashabiki wa Man United kuwasahau magwiji Andy Cole na Dwight Yorke.

5) Roque Santa Cruz - Blackburn (mabao 19, asisti 7)

Blackburn Rovers kwa sasa wanaendelea tu na desturi yao ya kunasa mastraika wa nguvu tangu walipopata huduma bora kutoka Roque Santa Cruz, aliyenaswa kutoka Bayern Munich mwaka 2007. Kwenye Ligi Kuu England, straika huyo wa Paraguay, alizidiwa na Cristiano Ronaldo, Fernando Torres na Emmanuel Adebayor kwa mabao kwenye msimu wake wa kwanza kwenye ligi hiyo baada ya kutumbukiza nyavuni mara 19 na kuasisti mara saba. Maisha yake huko Manchester City hayakuwa matamu, lakini kwenye kikosi cha Rovers, mambo yalikuwa tofauti kabisa - alionyesha kwamba yeye ni hatari kwenye msimu wa kwanza tu.

4) Fernando Torres - Liverpool (mabao 24, asisti 4)

Fernando Torres alikuwa hajulikani kabisa wakati anajiunga na Liverpool mwaka 2007, lakini kufika leo, anahesabika kama wachezaji wa kigeni waliofanya mambo makubwa kwenye Ligi Kuu England kutokana na ule uhodari wake wa kutikisa nyavu. Katika msimu wake wa kwanza, Torres aliweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kufikisha mabao 20 kwenye ligi akiwa na kikosi cha Liverpool tangu Robbie Fowler alipofanya hivyo. Alikuwa wa kwanza kupiga hat-trick katika mechi mfululizo, lakini Torres alionyesha kwamba yeye ni moto baada ya msimu wake wa kwanza kwenye Ligi Kuu England kufunga mabao 24 na kuasisti manne.

3) Kevin Phillips - Sunderland (mabao 30)

Kuna mengi ya kushangilia kwa Waingereza, lakini yote kwa yote ukweli utabaki palepale, straika Kevin Phillips alikuwa Mwingereza wa mwisho kubeba Kiatu cha Dhahabu cha Ulaya. Phillips alikuwa balaa sana katika msimu wake wa kwanza kwenye Ligi Kuu England akiwa na kikosi cha Sunderland, ambapo alifunga mabao 30. Staa huyo alipanda na timu kutoka Daraja la Pili hadi Ligi Kuu England na alionyesha moto wa juu si mchezo, akifunga mabao matata dhidi ya Chelsea, Leeds, Aston Villa na mahasimu wao Newcastle United.

2) Sergio Aguero - Man City (mabao 23, asisti 10)

Nyakati kali kabisa za Sergio Aguero kwenye kikosi cha Manchester City zilikuja mwishoni mwishoni mwa msimu wake wa kwanza kwenye Ligi Kuu England, lakini hata mwanzo alionyesha kwamba yeye ni straika wa kiwango cha dunia baada ya kunaswa na miamba hiyo akitokea Atletico Madrid. Mechi yake ya kwanza kabisa alifunga mara mbili na kuasisti mara moja dhidi ya Swansea City, kisha akafunga hat-trick dhidi ya Wigan, huku straika huyo Muargentina akifunga mabao 23 na kuasisti mara 10 katika msimu wake wa kwanza kwenye Ligi Kuu England.

1) Mo Salah - Liverpool (mabao 32, asisti 11)

Huu ni mwanzo bora zaidi kwenye Ligi Kuu England. Sawa, Mohamed Salah haikuwa mara yake ya kwanza kucheza kwenye Ligi Kuu England, kwani alikuwapo katika kikosi cha Chelsea - lakini mambo hayakuwa mazuri kupata nafasi kikosi cha kwanza Stamford Bridge. Alitimkia Italia kabla ya kurudi tena England na safari hii alitua huko Anfield kujiunga na Liverpool. Huko msimu wake wa kwanza kwenye Ligi Kuu England ulikuwa moto kwelikweli, alipofunga mabao 32 katika mechi 38. Alihusika pia kwenye asisti 11.