Bizimungu anukia Ihefu

SIKU mbili baada ya Ihefu kumtupia virago aliyekuwa kocha wao, Maka Mwalwisi, uongozi wa klabu hiyo umesema unatarajia kumtangaza kocha mpya wikiendi hii, huku jina la kocha wa zamani wa Mwadui, Ally Bizimungu likitajwa klabuni hapo.

Ihefu ilitangaza kumsitishia mkataba Mwalwisi akiwa ni kocha wa pili kufutwa kazi baada ya Zlatko Krmpotic aliyefurushwa Yanga baada ya mechi tano tu za Ligi Kuu Bara.

Afisa Habari wa Ihefu, Peter Andrew alisema uongozi wao unaendelea kupitia wasifu wa makocha walioomba kazi kwao na atakayekidhi vigezo atatangazwa mwishoni mwa wiki hii.

Juu ya Bizimungu, raia wa Rwanda kuwamo kwenye orodha hiyo, Andrew alikiri ni kweli wamepokea barua yake, ila kujua kama ndiye atakayepewa kazi ni ngumu kusema kwani watapitisha anayewafaa.

“Mchakato unaendelea kwa sababu majina yapo mengi kwa waliotuma maombi ya kazi akiwamo huyo Bizimungu, tunachosubiri ni uongozi kupitisha atakayetufaa” alisema Andrew.

Kwa upande wake Kocha Bizimungu aliiambia Mwanaspoti kuwa licha ya kwamba hajaongea na uongozi wa Ihefu, lakini yupo tayari kurudi Tanzania kwani ana uzoefu na soka hapa nchini.

“Kwa sasa nasubiri ofa yoyote kama wakinihitaji Ihefu niko tayari kwa sababu Tanzania ni kama nyumbani, nimefanya kazi huko muda mrefu nikiwa Mwadui FC, hivyo natamani kurudi,” alisema.