Huu moto wa Yanga hauzimwi

Muktasari:

HIVI unavyosoma sasa Yanga ipo kileleni! Hii ni baada ya kuibutua Kagera Sugar kwa bao 1-0 kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara, iliyopigwa jana kwenye Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba.

HIVI unavyosoma sasa Yanga ipo kileleni! Hii ni baada ya kuibutua Kagera Sugar kwa bao 1-0 kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara, iliyopigwa jana kwenye Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba.

‘Waleteni hao tuwapige’...Huu moto hauzimwi’...Ayaa sasa chongeni tena’... Hizo ni kelele za mashabiki wa Yanga waliosikika wakishangilia bao pekee na la ushindi lililofungwa na kiungo wao, Mukoko Tonombe dhidi ya Kagera Sugar kwenye mfululizo wa Ligi Kuu Bara.

Mchezo huo ulishuhudiwa Yanga ikipata ushindi wao wa pili mfululizo katika ligi hiyo na kufikisha jumla ya pointi saba na kuing’oa KMC iliokuwa ikiongoza tangu msimu ulipoanza ikiwa na alama zao sita.

Hata hivyo Yanga huenda ikaa kileleni kwa muda tu kwani leo kuna mechi tatu zinazohusisha timu zinazoweza kuing’oa ikiwamo ile ya Mbeya City dhidi ya Azam FC wakati Simba itaialika Biashara United, huku KMC yenyewe kesho Jumatatu itakuwa wageni wa Mwadui FC.

Licha ya kucharazwa nyumbani ikiwa ni kipigo chao cha pili kwenye Uwanja wa Kaitaba, lakini Kagera Sugar ilionyesha ushindani wa kweli kwa kuupiga mwingi kiasi cha kuwapa ugumu nyota wa Yanga ambao walimaliza dakika 45 bila kufanya maajabu.

Bao la kiungo fundi huyo kutoka DR Congo katika dakika ya 72, liliwapa jeuri mashabiki wa klabu hiyo wanaotamani mechi yao dhidi ya watani wa Simba, iliyopangwa kupigwa Oktoba 18 ipigwe hate leo ili kumaliza kelele mitaani.

Simba na Yanga zitavaana kwenye mechi ya mkondo wa kwanza ikiwa ni miezi kama mitatu tangu zilipoumana kwenye mchezo wa nusu fainali ya Kombe la ASFC na Jangwani kugarazwa kwa mabao 4-1 na kuwafanya mashabiki wao kupata fimbo ya kuwachapia mitaani.

Mukoko alifunga bao hilo akipokea pasi maridadi ya Mkongoman mwenzake, Tuisila Kisinda na kutuliza mpira kabla ya kuachia shuti kali kwa mguu wa kulia lililotinga nyavuni na kumuacha kipa wa Kagera Sugar, Ramadhan Chalamanda akiwa hana la kufanya.

Kama alivyofanya kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Mlandege ya Zanzibar walioifumua mabao 2-0, huku Tonombe akifunga la pili, Mukoko baada ya kufunga alikimbia hadi kwenye kibendera cha kona na kuwaita wenzake na kuwaambia wakae chini kisha kuonekana kama anawafundisha hivi, hivyo kuamsha shangwe kwa mashabiki waliohudhuria mchezo huo.

Licha ya Yanga kumiliki mpira kwa sehemu kubwa ya mchezo huo, lakini mambo yalikuwa magumu kwao kupata bao la mapema kutokana na uimara wa safu ya ulinzi ya Kagera Sugar iliyoongozwa na mabeki Erick Kyaruzi na Ally Mtoni ‘Sonso’, aliichezea Yanga msimu uliopita.

Yanga ilirejea kwa kasi zaidi kipindi cha pili hasa baada ya kufanyika kwa mabadiliko ya wachezaji akiingizwa Carlinhos na Deus Kaseke waliochukua nafasi za Kibwana Shomari na Yacouba Sogne, kwani wachezaji hao waliichangamsha safu ya mbele ya vijana wa Jangwani.

Katika kipindi cha kwanza timu zote zilishambuliana kwa zamu, huku Yanga wakionekana kumiliki mpira zaidi ya wapinzani wao, huku vita kubwa ikiwa eneo la katikati ya uwanja ambako kila timu ilijaza viungo mahiri.

Yanga ilianza na viungo Mukoko, Zawadi Mauya na Feisal Salum, huku Kagera ikiwa na Ali Nassoro Ufudu, Abdalah Seseme na Mohammed ‘MO’ Ibrahim’, japo kulikosekana ubunifu wa kuwatengenezea mabao washambuliaji mbali na kosa kosa za hapa na pale.

Dakika ya 44 Kagera ilikaribia kupata bao kama sio umahiri wa beki, Bakari Mwamnyeto kumwahi Erick Mwijage aliyekuwa akijiandaa kufunga bao mbele ya kipa Metacha Mnata.

Mara baada ya mchezo huo, Kocha wa Kagera, Mecky Maxime alisema wameumia kwa matokeo hayo kwani walicheza vizuri ila Yanga walitumia nafasi moja waliyioipata kuwaadhibu nyumbani.

“Mechi ilikuwa nzuri na tulikuwa na matarajio ya kushinda ili kurejesha morali katika kikosi changu baada ya kutopata matokeo mazuri michezo miwili iliyopita, ila bahati mbaya tumepoteza na huu hivyo lazima tujipe pole wote. Bado kuna michezo mingine bele naamini tutapata ushindi.

Naye Kocha wa Yanga, Zlatko Krmpotic amewapa hongera wachezaji wake kwa ushindi licha ya kukiri mchezo ulikuwa mgumu kwani Kagera Sugar ni timu nzuri.

“Tulitengeneza nafasi mbili tatu na kuweza kutumia moja hivyo nawapa hongera timu yangu kwa ushindi ingawa nahitaji kuona tukicheza vizuri zaidi katika michezo ijayo”, alisema Zlatko.

Katika mchezo huo, Yanga ililenga lango la Kagera mara moja tu, huku wenyeji wakifanya hivyo mara nne na kila timu ilipiga mashuti nje ya lango mara tisa.

Kagera ilipata kona tatu dhidi ya mbili za Yanga na ilicheza faulo mara 22 dhidi ya 18 za vijana wa Zlatko, huku ikiotea mara nne na Yanga ikifanya hivyo mara mbili, wakati kadi za njano Kagera ilipata mbili dhidi ya moja ya Yanga iliyotawala mchezo huo kwa asilimia 55 dhidi ya 45 za wenyeji hao waliosaliwa katika nafasi ile ile ya 14 waliokuwapo kabla ya mechi hiyo.

Vikosi vilivyoanza;

KAGERA;

Ramadhan Chalamanda, Mwaita Gereza, David Luhende, Ally Mtoni, Erick Kyaruzi, Ally Nassor, Ally Ramadhani, Abdallah Seseme, Hassan Mwaterema, Mohammed Ibrahim, na Vitalis Mayanga.

YANGA: Metacha Mnata, Kibwana Shomary, Yassin Mustafa, Lamine Moro, Bakar Mwamnyeto, Mukoko Tonombe, Zawadi Mauya, Feisal Salum, Michael Sarpong, Yacouba Songne na Tuisila Kisinda.

NAMUNGO YAPIGWA

Katika mechi nyingine ya ligi hiyo mapema, iliyopigwa Uwanja wa Nelson Mandela, mkoani Rukwa, Namungo ilijikuta kwa mara ya pili ikipasuka msimu huu baada ya kunyolewa na wenyeji wao Tanzania Prisons kwa bao 1-0.

Huo ulikuwa ushindi wa kwanza kwa Prisons na bao lao liliwekwa kimiani na Gasper Mwaipasi dakika ya 47 kwa shuti kali na kuipa timu yake pointi tatu za kwanza na kufika nne ikilingana na Simba, Polisi Tanzania na JKT Tanzania.

Imeandikwa na Oliver Albert na Mussa Mwangoka