Thiago kutua mwanangu, hao Chelsea wanalo hilo

Muktasari:

JURGEN Klopp amemnasa mtu wake, Thiago Alcantara na kila kitu kipo freshi kukipiga na Chelsea kwenye Ligi Kuu England leo huko uwanjani Stamford Bridge.

LIVERPOOL, ENGLAND

JURGEN Klopp amemnasa mtu wake, Thiago Alcantara na kila kitu kipo freshi kukipiga na Chelsea kwenye Ligi Kuu England leo huko uwanjani Stamford Bridge.

Liverpool imemnasa Thiago kwa mkwanja wa Pauni 20 milioni huku Pauni 6 milioni nyingine zitalipwa kulingana na ubora wa uwanjani wa mchezaji huyo, ambaye amesaini mkataba wa miaka minne wenye thamani ya Pauni 200,000 kwa wiki.

Ujio wa fundi huyo ambaye ni mtoto staa wa mpira wa Kibrazili, Mazinho kunafanya maisha ya Anfield kubadilika sana na kumfanya kocha Klopp kuwa na chaguo kadhaa ya fomesheni ndani ya uwanja.

Thiago kabla ya kutua Anfield alimuuliza, Philippe Coutinho kuhusu mabingwa hao wa Ligi Kuu England.

Beki wa zamani wa Manchester United na mpinzani mkubwa wa Liverpool, Gary Neville amesifu usajili huo wa Thiago na kusema: “Ni mchezaji wa kiwango cha dunia na atawapa Liverpool faida kubwa sana.”

Swali kubwa limeibuka Thiago atafiti wapi kwenye kikosi cha Klopp chenye viungo kibao, akiwamo Fabinho, Jordan Henderson, Gini Wijnaldum, Naby Keita, James Milner, Alex Oxlade-Chamberlain, pamoja na makinda Curtis Jones, Harry Wilson na Marko Grujic.

Kwa viungo waliopo, kabla ya kuja kwake, Liverpool imevuna pointi 196 ndani ya misimu miwili kwenye Ligi Kuu England. Ndani ya muda huo, Klopp amekuwa akitumia fomesheni ya 4-3-3.

Hiyo ndiyo fomesheni ambayo amekuwa akitumia, hasa kwenye mechi kubwa, ambapo Mohamed Salah na Sadio Mane wanacheza pande za pembeni kushoto na kulia ya Roberto Firmino, huku Trent Alexander-Arnold akicheza beki ya kulia na Andrew Robertson kushoto na viungo wa kati wamekuwa Fabinho, Henderson na wakati mwingine Wijnaldum ay Naby Keita. Ujio wa Thiago utaleta radha mpya kwenye kikosi hicho cha Klopp na uchezaji wake hauna tofauti na Jorginho wa Chelsea - kwamba siku zote mpira unapokuwa kwenye miguu yake basi kuna kitu atakifanya.

Ujio wake kwenye kikosi utawafanya Wijnaldum na Keita kuwa na wakati kwenye kupata nafasi, huko Klopp akiwa na machaguo mengine ya ziada ya mtindo wa kucheza ambao ni 4-5-1 na 3-5-2 kulingana na mpinzani wanayekabiliana naye.

Kocha Jurgen Klopp, alipokuwa Borussia Dortmund alikuwa akitumia fomesheni ya 4-2-3-1, kitu ambacho anaweza kukitumia kwa sasa baada ya kumpata Thiago, ambapo Mo Salah atatumika kwenye nafasi ya mshambuliaji wa kati.