Kagera ni mtu na mtu

Saturday September 19 2020

 

By SADDAM SADICK, MWANZA

WAKATI Kagera Sugar ikiwavaa Yanga leo Jumamosi, nahodha wa timu hiyo, Erick Kyaruzi amesema hawatamwachia mchezaji yeyote kufanya shambulizi ili kuhakikisha wanabaki na ushindi.

Timu hizo zinakutana huku Kagera Sugar ikiwa haijaonja ushindi katika mechi mbili za kwanza msimu huu baada ya kupoteza moja na sare moja, huku Yanga wakishinda moja na kupata sare moja.

Hata hivyo, rekodi zinaibeba Yanga katika dimba la Kaitaba hasa baada ya dimba la kuchezea kuwekwa nyasi bandia, ambapo katika mechi yao ya kwa ya dimba jipya, wenyeji ambao hapo awali walikuwa wakiwavimbia Yanga, walikumbana na kipigo kizito cha 6-2 Oktoba 22, 2016.

Na katika mechi yao ya mwisho msimu uliopita uwanjani hapo, ‘Wananchi’ walishinda bao 1-0 na kama haitoshi wenyeji wamekuwa wakipata matokeo yasiyoridhisha wawapo nyumbani.

Ikumbukwe kuwa hata mechi ya ufunguzi wa Ligi Kuu msimu huu, Kagera Sugar ikiwa nyumbani ilijikuta ikipoteza mbele ya JKT Tanzania bao 1-0, hivyo kuwafanya leo kuingia kwa tahadhari kubwa ili yasiwatokee tena.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kyaruzi alisema wanawaheshimu wapinzani wao, hivyo hawatamkaba mchezaji mmoja badala yake watacheza mtu kwa mtu ili kutoruhusu mashambulizi.

Advertisement

Alisema licha ya kwamba mechi ya mwisho hapo Yanga walipata ushindi, lakini hata hivyo Kagera Sugar ni moja ya timu iliyowapa shida sana msimu uliopita, hivyo wanaenda kupambana.

“Hatutamchunga mchezaji mmoja, tutacheza mtu na mtu, kwa sasa Yanga ni tofauti, lakini hata Kagera Sugar ni mpya, hivyo tunaenda kupambana bila kujali ya msimu uliopita,” alisema Kyaruzi.

Beki huyo aliongeza kuwa wamejiandaa vizuri na kwamba makosa waliyoyafanya katika mechi mbili zilizopita na kusababisha kukosa alama tatu, na yamerekebishwa.

Advertisement