Namungo Fc kujiuliza kwa Wajelajela

MWANZA. NAMUNGO FC ilipoteza mechi iliyopita ikiwa nyumbani dhidi ya Polisi Tanzania bao 1-0, sasa kocha wao Hitimana Thiery amesema hawatakubali kupoteza mchezo unaofuata baada ya hesabu zake kutibuliwa.

Hivi sasa, Namungo inakutana na maafande wa Magereza 'Prisons' katika mchezo wa raundi ya tatu utakaochezwa Uwanja wa Nelson Mandela mjini Sumbawanga, Jumamosi Septemba 19, 2020.

Namungo ilianza vyema mechi ya kwanza kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Coastal Union, haikuamini kilichowatokea kwa kulazwa 1-0 na Polisi Tanzania ambapo sasa wana kibarua kigumu ugenini.

Thiery amesema walikuwa na mkakati wa kushinda michezo yao yote ya nyumbani, kisha kuzigeukia za ugenini, hivyo baada ya mambo kutibuka sasa wanaenda kujiuliza kwa Tanzania Prisons.

Amesema anaamini mechi hiyo haitakuwa rahisi kutokana na wapinzani kuhitaji ushindi kwenye uwanja wao, hivyo watawakabili kwa umakini na tahadhari kubwa ili kufikia malengo yao.

“Tunaenda kupambana tena, hatuwezi kukata tamaa au kudharau mchezo, tumetoka kupoteza hivyo tunaenda na tahadhari ugenini malengo yetu ni kusahihisha makosa kupata pointi tatu” amesema Thiery.

Kocha huyo mwenye rekodi nzuri katika soka nchini, amefafanua kuwa uwezekano wa Namungo kuendeleza makali yake upo na kwamba ligi ndio imeanza na watafanya vizuri.

Amesema hata msimu uliopita wakiwa nyumbani walipoteza dhidi ya Coastal Union, hivyo hawawezi kutoka mchezo badala yake wanajipanga upya na mechi zinazofuata.

“Msimu uliopita tulipoteza dhidi ya Coastal Union tukiwa nyumbani lakini timu haikutetereka tukaendeleza makali yetu, hivyo hata msimu huu tutaendelea kutakata,” amesema kocha huyo raia wa Rwanda.