Fundi wa mpira aliyehama mtaa

Ukitaja kikosi cha wachezaji 11 matata kwenye Ligi Kuu ya wanawake Tanzania, basi lazima utakutana na jina la fundi wa mpira. Huyu ni Amina Ally Bilali wa Yanga Princess. Ni mahiri sana uwanjani na anacheza soka huku akilifurahia.

Amina ni kiungo matata ndani ya Yanga Princess ni moja ya wachezaji ambao warembo hao wa Jangwani wanajivuania sana baada ya kumuiba kutoka kwa watani zao, Simba Queens ambao ndio mabingwa wa ligi hiyo msimu uliopita.

Mbali na kuwa bora ndani ya timu yake, pia amekuwa msaada mkubwa katika timu ya Taifa ya Twiga Stars.

Mwanaspoti limezungumza na mkata umeme huyo asiyekuwa na mbwembwe na kuzungumzia mambo mbalimbali ikiwemo maisha yake ya soka huku akieleza kukerwa na tabia za baadhi ya wachezaji wenzake kujiweka kiume.

AIKACHA SIMBA

Amina anabainisha sababu zake za kuitosa Simba na kujiunga Yanga msimu uliopita huku akisisitiza maslahi ndio kila kitu.

“Simba Queens nimecheza msimu mmoja, na nilijiunga Yanga ambapo ndio timu yangu mpaka sasa. Kikubwa niliangalia maslahi kwanza ndio nikaondoka baada ya kuona dau la Yanga liko juu,”

CHANGAMOTO

Licha ya kukiri soka la wanawake kuzungukwa na mambo mengi, lakini soka lao kudharauliwa ni tatizo kubwa kwake hasa wakionekana kama watu wasioweza.

“Kwanza wanaume wanatuona kama hatujiwezi vile, basi wanakutenga, wakikuona unaingia uwanjani na kugusa mpira ndio wanaona unaweza, walau wanaanza kukuheshimu ila hili jambo sio zuri kabisa,” anabainisha.

KUJIWEKA KIUME

Watoto wa kike wengi wamekuwa na mtizamo usiokuwa sahihi wa kujiweka kiume kwa madai yao ya kucheza soka, lakini Amina anachukizwa na wenzake wanaojiweka hivyo.

Anasema, yeye ni mtoto wa kike na anatamani kuwa hivyo muda wote, hivyo hawezi kujibadilisha muonekano kwa kuwa anacheza soka na kwamba, hata dini yake haisemi hivyo.

“Hata nikisema nijiweke kiume kwanza haipendezi, mtoto wa kike ni wa kike tu na ina raha yake. Jamii yetu ya Kiafrika sio sawa, kwanza nimetoka familia ya dini.

“Napenda nibaki wa kike na tabia ya kike mpira haubadilishi jinsia yangu na sitaki hata unibadilishe muonekano hata kidogo,” anabainisha.

MPIRA NA ELIMU

“Kubalansi darasani na michezo ni mtihani, lakini nilijitahidi hata, Idd Kipingu anataka mchezaji ambaye anaweka maslahi ya elimu kwanza kisha ndio mpira ufuate,” anasisitiza.

Anasema Kipingu alikuwa mstari wa mbele kuwahimiza namna ya kupanga ratiba zao za darasani na uwanjani akiwa katika Shule yake Lord Baden Powell ili aweze kuvishika kwa pamoja kuepuka kupoteza kimoja wapo.

Amina anasema, kwa kutambua elimu ni muhimu na mpira bila elimu hauendi alijitahidi mpaka akamaliza kidato cha nne na ndipo alipoamua kuishia kwa sasa.

ATAKAVYORUDI DARASANI

Kwa sasa anakiri akili za darasani hana, ameamua kujikita katika soka, ndani ya muda ambao ataona unamfaa baada ya hapo atarejea darasani kujiendeleza.

“Kwa sasa elimu mwisho, lakini bado natamani huko mbeleni nijiendeleze tena katika masuala ya ujasiriamali ili niweze kujiajiri, habari za kuajiriwa nitaachana nazo nikiacha mpira,” anasema.

NDOTO ZAKE ZA NJE

Kila mchezaji anayesakata kabumbu iwe wa kiume au wa kike ukimuuliza juu ya malengo, atasema kucheza soka la kulipwa, hata Amina naye anatamani hilo kutokea.

Licha ya kutamani kufikia hatua hiyo, anapata hofu ya kufika huko kutokana na wachezaji wengi kwenda nje na kurudi kitendo kinachomfanya mguu mmoja ndani mwingine nje.

“Natamani kufika mbali kimpira kwa sisi wa kike ni mtihani sana kutoka hata wa kiume tunaona wanakwenda muda mfupi wanarudi Bongo, natamani kuitangaza nchi yangu ili nikipata nafasi ya kutoka nje,” anasisitiza.

FAMILIA YANYANYUA MIKONO

Wazazi wengi wamekuwa wakiweka ugumu kwa watoto wao wa kike kucheza soka, lakini baadaye hukubali matokeo baada ya watoto kuamua kukomaa na fani hiyo.

Hata kwa upande wake Amina yalimkuta, kwani baba yake mzazi alilazimika kunyanyua mikono juu baada ya kuona mwanaye asikii wala haambiwi kuhusu soka.

“Nilipata changamoto sana kuanzia shule nilikuwa naficha bukta yangu kwenye begi nikifika shuleni navua sketi navaa pensi, kwani baba alikuwa hataki kabisa kusikia mambo ya soka ilifikia nikawa namtoroka baba, alikuwa hataki nivae pensi.

“Nilikuwa nakaidi juu ya hilo mwishowe akaamua kukubali na kuona anachonizuia ndicho ninachokitaka, basi akawa mpole na maisha yakaendelea mpaka sasa ananisapoti tu”.

Anasema kuna siku alipokuwa akishiriki Mashindano ya Shule za Sekondari ‘Umiseta’ wakawa wanalipwa sh 30,000 anampelekea baba yake hapo ndipo alipoanza kuona mpira unalipa na kumsapoti.

“Si unajua familia zetu wacheza mpira wengi ni familia za chini, basi mzee alipopokea sh 30,000 alifurahi akaniambia kumbe mpira unalipa nikapata baraka zaidi,”

PACHA WAKE

Huwezi amini licha ya mapacha kutajwa kuendana tabia zao, lakini kwa hawa mambo sio hivyo kwani mwenzake alijaribu kutamani kuujua mpira ukamshinda kabisa.

“Peke yangu ndiye najua na napenda mpira, maana tuko mapacha na wote ni wasichana, ila mwenzangu alijaribu mpira ukagoma, akaamua kuacha.”

CHAMA, NIYONZIMA USIPIME

Licha ya Ligi Kuu Bara kuwa na wachezaji wengi, hasa viungo kama ya Amina, anasema wanaomkosha ni Clatous Chama wa Simba pamoja na Haruna Niyonzima wa Yanga.

“Nawakubali sana hawa wachezaji, wanavitu vyao adimu wawapo ndani ya uwanja, natamani nikipata nafasi ya kuonana na hawa watu wawili najua nitapata vitu vingi sana kutoka kwao, naimani ipo siku nitaonana nao,” anasema.

LIGI YAO

Anasema hapo awali ilizoeleka timu ya JKT Queens pekee ndiyo ambayo inatamba katika soka la wanawake, lakini sasa mambo yamebadilika na ushindani umekuwa mkubwa.

Anasisitiza kuwa msimu ujao ushindani utazidi kuongezeka kutokana na kocha wao kuyafanyia kazi mapungufu aliyoyaona hasa kupitia usajili kwa ajili ya kuboresha.

alikotoka

Msimu wa Mwaka 2012/13 akaenda Umisseta akitokea Kanda ya Mashariki, na ndipo Kanali Kipingu alipomuona na kumpeleka shule yake ya kukuza vipaji Lord Baden Powell iliyopo Bagamoyo.

Akiwa kidato cha pili alikuwa akiitumikia klabu ya Uzuri Queens na baadaye kutimkia Ever Green Queens.

Wakati huo huo alipata nafasi ya kuitumikia timu ya Taifa ya Vijana U-20 pamoja na Twiga Stars ambayo anaendelea kukipiga mpaka sasa.

Kwenye ligi alianza na Kigoma Sisters na kudumu misimu miwili, akajiunga Simba na msimu uliopita akatua zake kwa Warembo wa Jangwani.