Senga: Sioni beki wakuwakaba Tunombe, Kisinda

Muktasari:

Msanii wa vichekesho nchini, Alimarufu kama Senga amechekelea kuona uongozi wa Yanga umesajili vijana wadogo ambao watakaa nao kwa muda mrefu, amejigamba timu hiyo inakwenda kuwa mfano wa kuigwa ligi ya VPL.

USAJILI uliofanywa na Yanga msimu huu, umemkuna msanii wa vichekesho nchini, alimarufu kama Senga, anayetamba hakuna timu inayoweza kuzuia mvua ya mabao ligi ikianza Septemba 6.

Zimebakia siku mbili Yanga kufungua pazia la Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL), ambapo itacheza na Prisons, jambo ambalo Senga analisubilia kwa hamu kuona jinsi ambavyo timu hiyo itampa raha.

Senga anaamini huu ni msimu wa Yanga kurejesha heshima ya mataji Jangwani, baada yakuchukulia mara tatu mfululizo na wapinzani wao Simba.

"Simba walianza kicheko ila msimu huu watamaliza na kilio, Yanga imeleta majemba halafu vijana wadogo ambao wanajua kazi, hivi mfano Tuisila Kisinda na Mukoko Tonombe ni beki gani wa Simba ambaye anaweza akawazuia," amesema Senga nakuongeza kuwa.

"Natamani ligi ianze hata kesho, ili tujionee burudani halisi kutoka kwa majembe wa Jangwani, yaani nimefurahishwa sana usajili wa msimu huu unanipa kutembea kifua mbele,"amesema.

Senga amesema usajili wa msimu huu, anaona unalenga kuwa na timu bora ya muda mrefu, amesisitiza ndio maana uongozi umewachukua vijana ambao watakaa nao kwa muda mrefu.

"Unaona kabisa jinsi ambavyo timu inakuwa na malengo yakuona mbali, mfano uchukue wazee ambao baada ya muda unawaacha, Yanga inaenda kuwa ya tofauti kwenye ligi yetu, kikubwa vijana wetu watunzwe,"amesema.