Wawa hawahofii Onyango, Ame

Muktasari:

Beki wa Simba SC, Pascal Wawa amesema ujio wa wachezaji wapya ndani ya kikosi hicho, Joash Onyango na Ibrahim Ame umekoleza ushindani wa namba kwenye kikosi cha kwanza

Dar es Salaam. Beki wa Simba SC, Pascal Wawa amesema ujio wa wachezaji wapya ndani ya kikosi hicho, Joash Onyango na Ibrahim Ame umekoleza ushindani wa namba kwenye kikosi cha kwanza

Kwa sasa Simba inajumla ya mabeki watano wa kati akiwemo Wawa wengine ni Onyango, Ame, Erasto Nyoni na Kennedy Juma ambaye mwishoni mwa msimu uliopita alionekana kupata nafasi kubwa ya kucheza.

Wawa alisema amefurahishwa na ujio wa wachezaji hao ambao anaamini kwa ubora walionao wanaweza kusaidiana kuhakikisha Simba inaendelea kufanya vizuri.

“Nimekuwa nikienda changamoto na siku zote huwa naamini uwezo wangu hivyo sina presha ya namba na ninaami tutashirikiana vema kuhakikisha tunashinda mataji pamoja.

“Mambo ya harusi yameisha sasa huu ni muda wa kati na ninafuraha kurejea salama kuungana na wenzangu kwa ajili ya msimu ujao,” alisema beki huyo raia wa Ivory Coast.

Mwanzoni mwa msimu uliopita Wawa alikuwa akicheza na Nyoni kabla ya mambo kubadilika na kuanza kucheza na Kennedy.

Upande wa mke wa Wawa, Mertine alisema siku zote amekuwa akimsapoti mumewe kwa kumpa moyo ili aendelee kufanya zaidi, “Nimekuwa karibu naye huku nikitoa mchango wangu.

“Hii ni mara ya tatu nadhani kuwa Tanzania niliwahi kuwa huku kipindi ambacho alikuwa akiichezea Azam,” alisema.

Simba yapaa

Kikosi cha Simba kimeondoka jana jioni kwenda Arusha tayari kwa ajili ya mchezo wao wa Ngao ya Jamii dhidi ya Namungo.

Mchezo huo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, utakuwa ni wa ufunguzi wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2020/21, ambao utaanza rasmi Septemba 6.

Wapinzani wao, Namungo FC walianza safari asubuhi ya jana tayari kwa ajili ya mchezo huo wa Jumapili unaotarajiwa kuwa na upinzani. Simba imeifunga Namungo mara mbili na sare moja.