Morrison aahidi furaha Simba

Friday August 14 2020

 

By Charles Abel

SIKU chache baada ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kumpa uhuru wa kujiunga na timu aitakayo, winga Bernard Morrison amewaahidi furaha Simba sambamba na kuitumikia timu hiyo kwa nidhamu, utii na bidii.

Nyota huyo wa zamani wa Orlando Pirates na AS Vita, aliandika katika kurasa zake za mitandao ya Twitter na Instagram kuwa atahakikisha anafanya vyema ndani ya klabu ya Simba ili iweze kufanya vizuri.

"Nimetoka kuzungumza na bosi wa Simba Sports Club na nimemuahidi kuongoza kwa kuwa mfano bora, kuheshimu klabu na wanachama wake na kufanya kazi kwa bidii ili wawe na furaha.

"Nimefanya kazi na wengine kwa miezi minne lakini wakaja kugundua kuwa mimi ni mtu muda mfupi tu baada ya kujua kuwa nataka kuondoka. Wakaona sina nidhamu baada ya kutaka kuondoka lakini sikufanya lolote kwa yoyote yule.

"Kwenu nyie mashabiki wa Simba, nipo kwa ajili ya kubaki hapa. Nipo hapa kuwapa furaha. Nipo hapa kuwaheshimu na kuwawakilisha kwa vyovyote ninavyoweza. Sahauni kuhusu yoyote na tuifanye klabu yetu kuwa kubwa na ya kipekee," ameandika Morrison.

Jumatano, Agosti 12, Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF, ilimtangaza Morrison kuwa mchezaji huru na anaweza kujiunga na timu yoyote baada ya kubaini kuwa mkataba alioulalamikia na Yanga ulikuwa na mapungufu ya kisheria.

Advertisement

Mbali na hilo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Wakili Elias Mwanjala aliamuru mchezaji huyo kupelekwa mbele ya Kamati ya Maadili kwa kosa la kuidharau kamati yake kwa kusaini mkataba na Simba huku akiwa na shauri ambalo lilikuwa halijatolewa uamuzi.

"Kikao kilikuwa kirefu mpaka kufikia maamuzi haya, malalamiko ya Morrison yalikuwa kwamba hakuongeza mkataba na Yanga, tumeangalia mkataba wake tumeona una walakini  tumeona Yanga mkataba wao una utata kidogo,"

"Pia kuna mapungufu kwenye sehemu ya kusaini, imekatwa halafu hakuna sehemu ya waliosaini wote na kusema sheria inasema ukikata sehemu katika makaratasi basi inabidi umuite mwenzako asaini tena," alisema Mwanjala.

Advertisement