Kwa Mwamnyeto, Yanga yaipiga bao Simba hapa

Muktasari:

"Msimamizi wangu ndio kasimamia kila kitu. Nimesaini mkataba wa miaka miwili kwa Sh80 milioni" Mwamnyeto

MASHABIKI wa Simba, huenda bado hawaamini kama mabosi wao wamepigwa bao na wenzao wa Yanga katika dili la kumnasa beki Bakar Mwamnyeto aliyekuwa akiwindwa tangu msimu uliopita, lakini ukweli ndivyo ulivyo jamaa msimu ujao atavaa uzi wa kijani na njano baada ya kusaini miaka miwili.

Hata hivyo, wasichokijua mashabiki hao wa Msimbazi ni kwamba, mabosi wa Yanga walifanya umafia kwa kumwekea dau nono beki huyo wa kati na kumfanya asahau ahadi tamu na simu alizokuwa akipigiwa na matajiri wa Simba ili awatose Jangwani kwenda kucheza sambamba na Pascal Wawa.

Habari kutoka kwa mtu wa karibu wa beki huyo na kuthibitishwa na Mwamnyeto mwenyewe ni kwamba, dau la Sh 80 milioni alilowekewa mezani asaini mkataba wa miaka miwili Jangwani ndio lililomchanganya beki huyo mrefu na kuitosa Simba iliyokuwa ikimsumbua meneja wake, Kasa Mussa.

Usajili wa Mwamnyeto ndio ulioshtua zaidi kutokana na mchezaji huyo awali pia alikuwa anahitajika na Simba, lakini ghafla akabadilisha gia angani na kusaini mkataba wa kuitumikia Yanga na akizungumza na Mwanaspoti iliyotaka kujua ilikuwaje akabadilisha upepo ghafla, jamaa akafichua ukweli.

Awali, Mwamnyeto alisema kila kitu kiliinjiniwa na meneja anayemsimamia, Kassa Mussa aliyedai ndiye anayeweza kutoa majibu.

Lakini alipobanwa, beki huyo aliyekuwa pia nahodha wa Coastal na mmoja ya nyota 30 walioteuliwa kuwania Tuzo ya Mchezaji Bora wa msimu ulioisha, alisema hakuona sababu ya kuacha kusaini Yanga kutokana na ofa yake ambayo timu hiyo walikubaliana naye na kumuwekea mezani moja kwa moja.

“Msimamizi wangu ndio kasimamia kila kitu kwenye dili hili, lakini kwa ufupi ni kwamba nimesaini mkataba wa miaka miwili kwa Sh 80 milioni,” alisema mchezaji huyo ambaye alionekana kubanwa na msimamizi wake, kiasi cha kushindwa kujibu juu ya dau aliloahidiwa na Simba.

Hata hivyo, habari za mtu wa karibu wa mchezaji huyo aliidokeza Mwanaspoti kwa kudai kuwa hadi juzi alipotua jijini Dar es Salaam ili kumalizana na Yanga, mabosi wa Simba walikuwa wakimsumbua kwa simu yeye na meneja wake ili kutaka kupotezea dili hilo la Jangwani atue Msimbazi.

Inaelezwa kuwa Simba nao walikuwa wakikimbizana kumsaini Mwamnyeto na hawakutaka kukata tamaa ambapo simu za mabosi wao wawili (majina tunayo) walikuwa wakimsumbua meneja wa beki huyo Kasa Mussa kuwa waachane na Yanga kisha wakamalizane haraka akakipige Msimbazi pamoja na kina Wawa.

“Tulilazimika kumzuia Kassa na simu zake maana akitoka bwana mkubwa (anamtaja) anaingia mjumbe wake (anamtaja), lakini simu zao zilitusaidia na sisi kuongeza umakini na zoezi likamalizika na sasa Mwamnyeto ni mali ya Yanga baada ya kumalizana na klabu yake na yeye mwenyewe,” kilisema chanzo hicho.

MUUAJI WA SIMBA

Wakati Yanga, ikimalizana na Mwamnyeto na kisha kusikia Yusuf Mhilu waliyemtaka Jangwani amesaini mkataba Kagera Sugar, fasta wakaamua kumuibukia muuaji wa Simba na straika wa Mbao, Wazir Junior na kumalizana naye jijini Mwanza kwa kumsainisha mkataba wa miaka miwili.

Wazir ndiye aliyechangia kuilaza Simba kwenye mchezo wao wa marudiano wa Ligi Kuu Bara hivi karibuni uliopigwa Uwanja wa Taifa, wakati wakiwacharaza mabingwa hao mabao 3-2 na ushindi huo kuwasaidia kuepuka kushuka daraja moja kwa moja kabla ya kuanguka kwenye playoff mbele ya Ihefu ya Mbeya.

Wazir alithibitisha kufuatwa na mabosi wa Yanga asubuhi ya jana na kuzungumza nao kabla ya mchana wake kuamua kusaini mkataba wa miaka miwili.

“Awali nilijua nitatumiwa tiketi niwafuate Dar, lakini wameniibukia huku huku na kumalizana nao,” alisema straika huyo aliyemaliza ligi na mabao 13 kama Mhilu, lakini timu yake ikishuka daraja kwenye playoff.

Wazir anakuwa mchezaji wa tatu mzawa kutua Yanga baada ya Zawadi Mauya wa Kagera na Mwamnyeto ambaye kutua kwake kuna kila dalili za miongoni mwa mabeki wa kati ya timu hiyo kupigwa panga jangwani.

Kwa sasa Yanga ina mabeki wa kati sita akiwamo Lamine Moro, Said Makapu wenye mikataba yao, huku Kelvin Yondani na Andrew Vincent ‘Dante’ wao mikataba yao tayari imeshaisha. Pia inaye Ally Mtoni ‘Sonso’, Ali Ali na Sospter Cleophas.

Kama Junior atafanikiwa kujiunga na Yanga basi utakuwa usajili mzuri kwa Yanga kutona na mchezaji huyo kuwa na uwezo mkubwa wa kufunga anapokuwa yupo mbele ya lango, pia watakuwa wamewatibulia Azam walikuwa wakitaka kumrejesha kikosini.

BEKI WA JESHI ACHANA MKATABA

Katika hatua nyingine inaelezwa kitendo cha Yanga kumsajili beki wa pembeni wa Polisi Tanzania, Yassin Mustafa umefuta usajili wa staa mwingine wa kigeni aliyekuwa akihesabiwa siku kutua nchini.

Awali Yanga ilikamilisha usajili wa beki raia wa Rwanda, Eric Rutanga aliyeliambia Mwanaspoti tayari alishatumiwa mkataba na alishausaini.

“Nilishasaini mkataba wa miaka miwili kwasasa nasubiri tiketi ya ndege tu nije huko Tanzania ndio maana unaona sasa nafanya mazoezi makali,” alisema Rutanga beki wa zamani wa APR na Rayon Sport zote za Rwanda.

Hata hivyo, wakati Rutanga akisubiri tiketi hiyo huku nyuma Yanga wakabadili hesabu na sasa wamemsajili Mustafa.