Ile vita ya usajili yaanza rasmi

Saturday August 1 2020

 

By KHATIMU NAHEKA

SIMBA, Yanga na Azam zimeshaanza rasmi kufanya usajili mpya kwa msimu ujao wa Ligi Kuu Bara, lakini haikuwa rasmi mpaka leo ambapo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limefungua rasmi dirisha la usajili kwa Ligi zote kubwa taarifa imesema.

Taarifa iliyotolewa na TFF kupitia ofisi ya Afisa Habari wao Clifford Ndimbo imesema dirisha hilo limefunguliwa rasmi leo Agosti Mosi kwa klabu za Ligi Kuu,Ligi Daraja la kwanza na ligi daraja la pili na Ligi kuu ya wanawake.

Taarifa hiyo imesema kuwa usajili huo utafanyika kwa muda wa mwezi mmoja na dirisha litafungwa Agosti 31 saa 5:59 usiku.

TFF imezitaka klabu zote kama zitakutana na changamoto zozote ziwasiliane na Shirikisho hilo kwa idara ya mashindano ya TFF.

Aidha TFF imezikumbusha klabu zote kuwa hakutakuwa na muda wa kuongeza katika usajili huo endapo muda wa sasa utakamilika ambapo wote wanatakiwa kukamilisha usajili kwa wakati.

Wakati TFF ikitangaza dirisha hilo, tayari klabu ya Azam, imesawasajili wachezaji wawili na kuwatambuilisha akiwamo Awesu Awesu kutoka Kagera Sugar, huku Yanga ikimalizana rasmi na Zawadi Mauya pia kutoka Kagera Sugar na watani zao Simba wamembeba David Kameta 'Duchu kutoka Lipuli na tayari Jangwani ipo hatua ya mwisho pia kumsainisha beki Bakar Mwamnyeto wa Coastal Union.

Advertisement

 

Advertisement