Simba, Yanga nusu fainali FA

Wednesday July 1 2020

 

By Khatimu Naheka

SIMBA imeupiga mwingi ikipata ushindi mwanana wa mabao 2-0 mbele ya Azam FC na kufanikiwa kuwafuata watani wao Yanga katika hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho.

Ushindi huo wa Simba ni kama imewaambia Yanga ambao juzi walitinga hatua hiyo kwa kuichapa Kagera Sugar kwa mabao 2-1, ambapo Wekundu hao watakuwa na akili moja tu ya kutaka kulipa kisasi mbele ya Yanga baada ya kuchapa katika ligi.

Mabao mawili kila kipindi yalitosha kabisa kuipa Simba ushindi huo muhimu huku wakionekana kuwabana vyema Azam ambao walionekana kuwa baridii karibu muda wote wa mchezo.

Kipindi cha kwanza hakikuwa na utengenezaji mkubwa wa  nafasi za kutafuta mabao ambapo timu zote zilionekana kucheza sana eneo la kati lakini safu za ulinzi zikionekana kuwa na utulivu mkubwa kudhibiti mashambulizi.

Simba dakika ya 11 kipa wa Azam Benedict Haule alifanya kazi nzuri kuzuia krosi ya Luis Miquissone akimtafuta nahodha wake John Bocco aliyekuwa nyuma akiisubiri mvuke kipa huyo lakini ikadakwa vyema wekundu wakifika vyema lango la wapinzani wao.

Dakika ya 28 Miquissone alipoteza nafasi nzuri shuti lake kali Haule anapangua na mabeki kuokoa akipokea pasi ya Francis Kahata Simba ikitengeneza shambulizi zuri kupitia mpira wa adhabu ndogo.

Advertisement

Simba ilifanikiwa kupata bao la kwanza dakika ya 39 mfungaji akiwa Bocco kwa kichwa safi akipokea krosi safi ya Kahata baada ya Azam kupoteza mpira kirahisi na wekundu hao kufanya shambulizi la haraka.

Kuingia kwa bao hilo kidogo kukawaamsha Azam na kwa mara ya kwanza dakika ya 41 walifika lango la Simba vizuri lakini shuti kali ya mshambuliaji Richard Djodi linapanguliwa na kipa Aishi Manula kisha mabeki wakaokoa.

Dakika ya 45 Simba ilipata pigo beki wake Kennedy Juma aliumia baada ya kukanyagwa na mshambuliaji wa Azam Obrey Chirwa na kutolewa nje kwa matibabu na hata hivyo hakuweza kurejea tena uwanjani.

Mpaka mapumziko Simba ilitoka kifua mbele kwa bao hilo 1-0.

Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kufanya mabadiliko Simba wakimuingiza Erasto Nyoni akichukua nafasi ya Juma aliyeumia huku Azam bao wakimtoa kiungo Mudathir Yahaya nafasi yake ukienda kwa Bryson Raphael.

Dakika ya 47 Simba waliendelea kuliandama lango la Azam beki wake wa kulia Shomari Kapombe alipoteza nafasi nzuri akishindwa kumfunga Haule akipokea pasi ya Clatous Chama na kuwa kona ambayo hata hivyo kichwa cha Gerson Fraga kikapaa juu kidogo.

Dakika ya 52 Never Tigere alipoteza nafasi nzuri shuti lake la mpira wa adhabu ndogo linapanguliwa na Manula kisha mabeki wanaokoa

Dakika ya 54 Simba waliandika bao la pili likifungwa na Chama shuti lake kali likigonga mwamba wa chini kisha kujaa wavuni akipokea pasi safi ya Kapombe.

Azam hawakuonekana kama wamekuja kutafuta ushindi kwa kukosa kasi mbele Simba.

Dakika ya 56 Miquissone alipoteza nafasi nzuri kuipatia timu yake bao la tatu shuti lake kali Haule analipangua na kudaka tena.

Baada ya mabao hayo Simba walionekana kuuchezea mpira wakiwasubiri Azam waje lakini nao hawakuonekana kuhitaji kushambulia zaidi.

Mpaka mwisho wa mchezo Simba iliondoka kifua mbele kwa ushindi huo wa mabao 2-0 na sasa watakutana na Yanga katika hatua ya nusu fainali, huku Namungo watavaana na Sahare All Stars walioing'oa Ndanda katika mechi yao ya mapema leo iliyoamuliwa kwa penalti.

Advertisement